Serikali imetangaza kuzifutia usajili
meli mbili zilizokamatwa zikisafirisha dawa za kulevya na silaha na
kuzitaka kushusha bendera ya Tanzania.
“Tumefuta usajili wa meli
hizo na kuwataka kushusha bendera yetu na wapambane na tatizo hilo wao
wenyewe na sisi tutatoa ushirikiano wote utakaohitajika,” amesema Makamu wa Rais Samia Suluhu.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Rais, samia
Suluhu Hassan, alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo, Januari
18, 2018 Ikulu, jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa licha ya kuzifutia
usajili, hatua nyingine zinaendelea ili kuwabaini wahusika halisi.
Makamu wa Rais amezitaja meli hizo kuwa
ni Kaluba yenye usajili namba IMO 6828753 iliyokamatwa huko Jamhuri ya
Dominican Desemba 27, 2017 ikiwa na shehena ya dawa za kulevya zenye
uzito wa kilogramu 1,600, na nyingine ni ni Andromeda yenye usajili IMO
7614666 iliyokamatwa ikisafirisha silaha kwenda nchini Libya kinyume
cha sheria za Kimataifa.
Ameeleza kuwa meli hizo zilisajiliwa
Tanzania kupitia taasisi ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar ambayo
ndiyo imepewa mamlaka ya kusajili meli zote za nje.
“Wanaposajili wanajaza fomu
mbili ikiwepo moja ya kiapo cha kutokujihusisha na biashara ya dawa za
kulevya, silaha au watu. Kwa wao kufanya hivyo wamekiuka kiapo
walichoapa,” amesema Makamu wa Rais.
Ameendelea kusema kuwa baada ya tukio
hilo Rais Dkt. John Pombe Magufuli alimwagiza kufanya kikao na Serikali
ya Zanzibar, kikao ambacho kimetoka na mapendekezo kadhaa ikiwamo kuunda
kamati maalum ya kupitia usajili wa meli zote pamoja na sheria za
usajili na kodi.
Makamu wa Rais amesema katika kikao
hicho kilichofanyika Zanzibar kilihudhuriwa na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd na viongozi wengine na wamekubaliana
kuunda kamati maalum itakayoshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama
kuanza mchakato wa kupitia meli zote zilizosajiliwa na zitakazosajiliwa
kuona umiliki wake.
No comments:
Post a Comment