Serikali imewasilisha Mkataba wa
Kimataifa wa Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika
Mashariki kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Akiwasilisha Mkataba huo kwa niaba ya
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa
Tanzania na Uganda ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo
malengo yake ni pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama
kwenye maeneo ya kisiasa, kiuchumi, kijamii kiteknolojia , utafiti,
ulinzi na masuala ya Kisheria.
Dkt. mwakyembe amesema kuwa Serikali
ya Uganda kupitia kampuni za Kimataifa za TOTAL, TULLOW NA CNOOC
iligundua uwepo wa mafuta ghafi takribani mapipa bilioni 6.5 katika eneo
la Albertine nchini Uganda.
“Kufuatia ugunduzi huo, Serikali
ya Uganda ilianza kutafuta njia ya kusafirisha mafuta hayo kwenda kwenye
soko la kimataifa ambapo iliaanisha njia takribani tatu ikiwemo ile ya
kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania,” amesema Dkt. mwakyembe.
Aidha Dkt. mwakyembe amebainisha
baadhi ya faida zitokanazo na Mkataba huo ikiwemo kuongezeka kwa mapato
ya Serikali kutokana na Kodi ya zuio na Kodi ya Mapato ya Kampuni
zitakazotozwa wakati wa ujenzi na uendeshaji wa Mradi.
Vilevile amesema kuwa Serikali ya
Tanzania itanufaika katika kuongezeka kwa mapato ya Serikali kwa
takribani Dola za Marekani 12.2 kwa kila pipa la mafuta ghafi
litakalosafirishwa kupitia Bandari ya Tanga kulingana na kiwango cha
Hisa za Serikali ya Tanzania.
“Kuimarika kwa mahusiano ya
kidiplomasia, ulinzi na usalama kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na Jamhuri ya Uganda pamoja na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa
ujumla sambamba na kuimarika kwa huduma mbalimbali katika bandari ya
Tanga kutokana na shughuli za Mradi na miundombinu itakayojengwa,” aliongeza Dkt. Mwakyembe
Pia ongezo kwa fursa za ajira kwa
Watanzania ambapo takribani watanzania 10, 000 wataajiriwa wakati wa
ujenzi na ajira zipatazo 1,000 wakati wa uendeshaji, Amesema Dkt.
Mwakyembe.
Kwa upande wake Deogratius Ngalawa
akimuwakilisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini ameishauri Serikali kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa mkataba
huo kwa kuzingatia mustakabali wa manufaa ya kiuchumi kwa Taifa.
“Napenda kutoa pongezi za dhati
kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa
juhudi zake na umahiri aliouonesha katika kuhakikisha Tanzania inapata
fursa ya mradi huu mkubwa wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi
kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania,” amesema Ngalawa.
Akiongea kwa niaba ya Msemaji Mkuu
kambi Rasmi ya Upinzani Wizara ya Nishati na Madini Mhe. Devota Minja
amesema kuwa bomba hilo la kusafirisha mafuta ilikuwa na kazi iliyohusu
zaidi ushawishi mpana kwani kulikuwa na ushindani mkubwa utoka kwa nchi
jirani.
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma
No comments:
Post a Comment