Wakili Hudson Ndusyepo
WATU wasiojulikana waliovunja ofisi za
mawakili wa Prime Attorneys ambayo pia inashughulikia kesi ya Yusuf
Manji wameiba Sh3.7 milioni na nyaraka kadhaa zikiwamo hati za viwanja.
Hata hivyo, nyaraka za kesi ya
mfanyabiashara huyo zimesalimika, huku msemaji wa ofisi hiyo wakili Asia
Charli akisema licha ya jengo hilo kuwa na ofisi mbalimbali kama
maduka, saluni na gym ni ofisi yao tu iliyopo ghorofa ya tatu ndiko
kumeibwa nyaraka na fedha.
Ofisi za kampuni hiyo zipo jengo la
Prime House lililopo Mtaa wa Tambaza, Upanga jijini Dar es Salaam jirani
na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Ilala.
Katika wizi huo, watu hao wasiojulikana waliiba kasiki lenye fedha na nyaraka. Hilo
ni tukio la pili kwa ofisi za mawakili katika siku za karibuni
kufanyiwa uhalifu, baada ya kampuni ya Immma Advocates kushambuliwa na
kitu kilichodaiwa kuwa bomu na kuteketea kwa baadhi ya nyaraka.
Akizungumzia tukio la kuibwa kwa fedha
na nyaraka katika ofisi yao, Charli alisema jana kuwa: “Nyaraka
mbalimbali za wateja na zetu zimechukuliwa na ni za muhimu sana.”
Alisema nyaraka kuhusu kesi za mfanyabiashara Manji anayewakilishwa na
kampuni hiyo zilisalimika.
Wakili katika ofisi hiyo, Hudson
Ndusyepo ambaye ni miongoni mwa mawakili wanaomtetea Manji katika kesi
ya uhujumu uchumi, alisema kabla ya wizi huo waliohusika walimfunga
kamba mlinzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum
Hamduni alisema tukio hilo lilitokea kati ya saa nane na tisa usiku wa
kuamkia jana na uchunguzi unaendelea.
Katika tovuti yake, Prime Attorneys inaeleza kuwa ilianzishwa mwaka 2010.
Awali jana asubuhi mwandishi wa
Mwananchi alishuhudia barabara ya kuingia zilipo ofisi za kampuni hiyo
ikiwa imefungwa kwa muda na polisi ambao walitumia magari yao kuziba
njia na kuweka uzio wa utepe wa rangi ya njano.
Mmiliki wa saluni ya Posh Unisex, Fatma
Ebrahim alisema katika uvamizi huo, pia mlango wa saluni yake wenye
thamani ya Sh2.5 milioni ulivunjwa lakini hakuna mali iliyoibwa.
Kwa sasa siwezi kusema wahalifu hawa
walilenga ofisi gani maana zipo nyingi katika jengo lile. Naomba mtupe
nafasi tufanye uchunguzi kisha tutawapa taarifa.
No comments:
Post a Comment