Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa Ndg Herry James
akisalimiana na baadhi ya viongozi wa UVCCM Mkoa wa Arusha mara baada
ya kuwasili Mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ya siku mbili. Picha Na
Mathias Canal
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)
Taifa Ndg Herry James amesifu ushirikiano wa wananchi Mkoani Arusha kwa kuunga
mkono juhudi za serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli katika kusimamia rasilimali za
Taifa.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM
ameeleza hayo Mara baada ya kuwasilia Mkoani Arusha leo 10 Januari 2018 katika
ziara yake ya kikazi ya siku mbili ambapo pamoja na mambo mengine atashiriki
kampeni za kumnadi Mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Longido katika uchaguzi mdogo
unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Akizungumza na Vijana wa Chama Cha Mapinduzi waliozuru kumlaki
katika Mtaa wa Tengeru, Wilaya ya Meru, Herry aliwasisitiza Vijana hao
kuendeleza mahusiano mazuri kwa Chama na serikali ili kuwa na jamii yenye
nidhamu, weledi na mtazamo chanya katika utendaji.
Alisema pia mahusiano mazuri ndio msingi wa ushindi wa ngazi
mbalimbali ikiwemo uchaguzi mdogo wa udiwani uliomalizika hivi karibuni na CCM
kuibuka kidedea kwa zaidi ya asilimia 97%.
Aidha, Herry amewafikishia vijana hao salamu za Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa kuwa
amemuelekeza kushiriki kampeni za Uchaguzi mdogo ambapo pamoja na mambo mengine
Rais Magufuli anatarajia matokeo ya ushindi wa kishindo katika chaguzi zote za
marudio nchini.
Aliongeza kuwa katika kipindi kirefu Mkoa wa Arusha umekuwa na
viongozi wasiokuwa na maamuzi lakini kupitia serikali ya awamu ya Tano viongozi
wengi wamekuwa na maamuzi muhimu na mazuri kwa wakati sahihi huku akisifu
uwajibikaji wa Kamishna wa CCM Mkoa wa Arusha ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo
Mhe Mrisho Gambo.
Sambamba na hayo pia amewasihi Vijana wote nchini kusimamia kile
wanachokiamini kwa maslahi ya wengi na kuwa na maamuzi yakinifu kwa wakati
sahihi.
No comments:
Post a Comment