Uchaguzi Mdogo wa majimbo ya Siha
mkoani Kilimanjaro na Kinondoni mkoani Dar es Salaam pamoja na
Kata nne za Tanzania Bara utafanyika tarehe 17/02/2018, kufutia
waliokuwa Wabunge katika majimbo hayo kujivua Uanachama na kukosa sifa
za kuendelea kuwa wabunge.
Taarifa ya Makamu Mwenyekiti wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Hamid Mahmod
Hamid imeeleza kuwa pamoja na Majimbo hayo,pia Kata nne za Isamilo
katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza,
Manzase Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Madanga
Halmashauri ya Wilaya ya Pangani mkoani Tanga na Kimagai
Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma zitafanya Uchaguzi
mdogo
Aidha,
Jaji Mkuu (Mst. Zanzibar) Hamid Mahmoud Hamid amesema kuwa,
Tume inaendesha uchaguzi huo baada ya kupokea barua kutoka kwa
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mh. Job Ndugai kuhusu
uwepo wazi wa jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam na
Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro.
Jaji Mahmoud amesema kuwa, barua
hiyo ilieleza kuwa majimbo hayo yapo wazi baada Maulid Mtulia
aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kujivua uanachama wa
CUF na Dr. Godwin Mollel wa jimbo la Siha kujiuzulu uanachama
wa CHADEMA na hivyo wote kukosa sifa za kuwa Wabunge.
Pia, ameeleza kuwa Tume ilipokea
taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa
ikiitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Udiwani katika kata
nne za Tanzania Bara
“Baada ya kupokea barua hizo
Tume kwa kuzingatia vifungu vya 37(1) na 46(2) vya Sheria ya
Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 pamoja na kifungu cha 13(3)
cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa sura ya 292
inatangaza kuwa majimbo mawili na kata nne zipo wazi,” alisema Jaji Mahmoud.
Ameeleza kuwa, fomu za uteuzi kwa
majimbo hayo mawili na kata nne itakuwa kati ya tarehe 14 –
20 Januari, 2018, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe
20/01/2018, na Kampeni za uchaguzi mdogo zitafanyika kuanzia
tarehe 21/01 – 16/02/2018 na siku ya uchaguzi itakuwa tarehe
17/02/2017.
Vilevile, Jaji Mahmoud
amevikumbusha Vyama vya Siasa na wadau wote wa uchaguzi
kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo yote
wakati wa uchaguzi huo mdogo.
Subira Kaswaga, NEC
No comments:
Post a Comment