WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA 2017:WANACHAMA,WATEJA WAPEWA HUDUMA YA ZIADA KATIKA KUADHIMISHA - TANZA MEDIA ONLINE

Thursday 5 October 2017

WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA 2017:WANACHAMA,WATEJA WAPEWA HUDUMA YA ZIADA KATIKA KUADHIMISHA

Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani wa PSPF, Bi. Costantina Martin, akipitia taarifa za Mteja aliyefika kuhudumiwa.

WATEJA wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF wanaofika kwenye ofisi za makao makuu jengo la Jubilee Tower jijini Dar es Salaam ili kujipatia huduma katika kipindi hiki cha Wiki ya Huduma Kwa Wateja Duniani, wamekuwa wakifaidika na huduma za ziada zinazotolewa na washirika wa Mfuko huo ambao wameweka kambi kwenye eneo hilo.

Washirika wa Mfuko walioweka kambi kwenye ofisi hizo tangu Otoba 2, 2017, ili kuwahudumia wateja ambao ni pamoja na Wastaafu na Wanachama wa PSPF ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, (NHIF), Benki ya CRDB, Benki ya Posta Tanzania, (TPB), Benki ya NMB na Mwalimu Commercial Bank Plc (MCB), Menenja wa Huduma kwa Wateja wa PSFP, Bi. Laila Maghimbi amesema.
 
Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa wateja, Mfuko wa Penshini wa PSPF, Bi. Queen Edward, akiwaeleza wateja hawa wa Mfuko huo, kuhusu huduma za ziada zinazopatikana kweye eneo hilo.
Maafisa waandamizi wa PSPF, Bw. Gabriel P.Maro, (kushoto) na Bw. Abdul Njaidi wakifurahia jambo

“Kama mnavyoona, mwaka huu tumeamua kuongeza huduma za ziada kwa wateja wetu, yaani wastaafu na wanachama wanaofika kupatiwa huduma ofisini kwetu, ambapo Mteja baada ya kuhudumiwa pia anaweza kuonana na washirika wetu, ambapo NHIF wanafanya uchunguzi wa afya bure, mabenki nayo yapo hapa kuwaelimisha kuhusu jinsi wanavyoweza kuweka fedha zao na kupatiwa mikopo nafuu ili kuendesha miradi mbalimbali na hivyo kujiongezea kipato.” Alifafanua Bi. Maghimbi.

Alisema, nia ya Mfuko ni kuhakikisha wanafurahia huduma zitolewazo lakini pia kuonyesha kuwajali wateja wao kwa kuwasogezea karibu huduma muhimu za afya na kibenki.

Wateja wamekuwa wakifurika kwenye ofisi hizo tangu Wiki ya Huduma kwa Wateja ianze Oktoba 2, 2017 na miongoni mwa huduma zitolewazo ni pamoja na wastaafu kufuatilia taarifa za michango yao, kuhakikiwa, kulipwa mafao na kusajili wanachama wapya kupitia Mpango wa Uchangiaji wa Hiari, (PSS).

Aidha wanachama wanaofika kwenye ofisi hizo wamekuwa wakipatiwa maelezo ya namna wanavyoweza kupatiwa mikopo ya viwanja na nyumba za makazi ambapo kampuni mshirika ya PSPF, Ardhi Plan Limited kupitia afisa wake, Bi.Anna Lukindo imekuwa ikifanya kazi hiyo.

No comments:

Post a Comment