WAFARIKI KWA UNYWAJI WA POMBE HARAMU YA GONGO - TANZA MEDIA ONLINE

Thursday 5 October 2017

WAFARIKI KWA UNYWAJI WA POMBE HARAMU YA GONGO

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA
POLISI KANDA MAALUM DSM
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
05/10/2017
POMBE YA KIENYEJI AINA YA GONGO YAUA WATU KUMI (10)
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm mnamo tarehe 04/10/2017 majira ya saa kumi kamili alfajiri lilipokea taarifa kutoka kwa mwananchi aitwaye MATIGO RAMADHANI (38) mkazi wa Kimara Stop over kuwa tarehe 03/10/2017 majira ya saa kumi na moja jioni ndugu yake aitwaye MALEO RAMADHANI (45) mkazi wa Stop over alirudi nyumbani akilalamika kuumwa tumbo, kuishiwa nguvu na kizunguzungu na kumweleza alikunywa pombe ya kienyeji kwa mama aitwaye ANOZA. Alimpeleka Hospitali ya Mwananyamala na baada ya kupata matibabu alirudi naye nyumbani na hatimaye alifariki dunia usiku.
Baada ya muda alijitokeza mtoa taarifa mwingine aitwaye PAULA KISANGILA (53) mkazi wa Stop over alieleza kuwa aliporudi nyumbani kwake kutoka kwenye shughuli zake majira ya saa tano usiku hakumkuta mlinzi wake ajulikanaye kwa jina moja la YONA umri kati ya miaka 20-30 mkazi wa Stop over walijaribu kumtafuta na baadae walimkuta akiwa amefariki nje ya uzio.
Aidha taarifa nyingine zilipatikana kuwa kuna watu wengine saba wamefariki dunia kwa kunywa pombe hiyo ya kienyeji na miili yao ipo katika Hospitali ya Mwananyamala na hospitali ya Tumbi Kibaha ,majina yao ni;
  1. MOHAMED ISSA miaka 67, mkazi wa Kimara Saranga
  2. KABUGI RASHIDI miaka 64, mkazi wa Kimara Saranga
  3. STANSLAUSI JOSEPH miaka 58, mkazi wa Kimara Saranga
  4. STEPHEN ISAYA miaka 61, mkazi wa Kimara Saranga
  5. MONIKA RUGAILLUKAMU miaka 42, mkazi wa Kimara Saranga
  6. ALEX MADEGA miaka 41, mkazi wa Kimara Korogwe
  7. HAMISI MBALA miaka 35,mkazi wa Kimara Golani
  8. EKSON NYONI miaka 28, mkazi wa Kimara Stop over

Upelelezi wa awali uliweza kubaini kuwa eneo la tukio lililokuwa linauzwa pombe ya kienyeji ni eneo la Kimara Stop Over na mtu aliyekuwa akiwauzia pombe marehemu hao anajulikana kwa jina la mama ANOZA, na katika eneo la tukio ziliokotwa chupa tatu za ujazo wa lita moja zikiwa zimejazwa pombe inayodhaniwa kuwa ni pombe ya moshi (gongo).
Vielelezo vyote vinapelekwa kwa mkemia mkuu wa serikali ikiwa ni pamoja na miili ya watu waliokufa ili kufanyiwa uchunguzi na kubaini chanzo halisi cha vifo hivyo, huku msako mkali ukiendelea kufanyika ili kumkamata mtuhumiwa huyo aliyewauzia pombe kwa hatua za kisheria.
L.B.MAMBOSASA – SACP
KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM

No comments:

Post a Comment