MFANYABIASHARA maarufu nchini, Yusuf Manji ameachiwa huru katika kesi
ya madawa iliyokuwa ikimkabili baada ya mahakama kushindwa kuthibitisha
madai hayo.
Akisoma huku hiyo Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Cyprian Mkeha amesema mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya
upande wa mashtaka kushindwa kutoa ushahidi wa kujitosheleza hivyo
mahakama hiyo kushindwa kuthibitisha iwapo Manji anatumia madawa ya
kulevya.
Aidha Mkeha ameeleza kuwa mahakama imejiridhisha kuwa mtuhumiwa
alikuwa bado anatumia dawa mbalimbali kwa matibabu yake kulingana na
maagizo ya daktari na dawa hizo zina vimelea vya morphine ambayo pia
inaweza kukutwa kwenye heroine, kwa hiyo maabara ya Mkemia Mkuu
ingeenda mbele zaidi kujua morphine iliyokutwa kwa mtuhumiwa imetokana
na nini?
Hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, Cyprian Mkeha alitumia zaidi
ya saa moja kusoma hukumu hiyo akiichambua kesi tangu mshitakiwa huyo
alivyokamatwa mpaka alivyochukuliwa kipimo cha mkojo.
Baada ya kueleza hayo hakimu huyo aliuchambua ushahidi uliotolewa kwa
pande zote mbili ambapo alihitimisha kwa hukumu ya kumuachia huru
mshitakiwa.
Hukumu mhiyo ilizua mayowe ya furaha na kukumbatiana kwa kupongezana ambapo mahakama hiyo iligubikwa na furaha kila kona.
Manji baada ya kuachiwa huru wanahabari walitaka kuzungumza naye
lakini watu wake wa karibu walimzuia kufanya hivyo na kumkimbiza kwenye
gari na kumuondoa eneo hilo.
Kufuatia hukumu hiyo mwanahabari wetu alizungumza na wakili wa
Serikali aliyekuwa akisimamia kesi hiyo, Nassoro Katuga na kutaka kujua
wanavyoipokea hukumu hiyo.
“Ukweli sisi hatukubaliani na hii hukumu ni lazima tukate rufaa kwani mahakama imetupa siku 30, za kukata rufaa kama hatukubaliani na hukumu.
Hivi unavyotuona tunasubili nakala ya hukumu ili tuanze mchakato wa kukata rufaa.
Manji alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Februari 16, 2017 akituhumiwa kwamba, kati ya Februari 6 na 9, 2017 katika eneo la Upanga Sea View, Ilala alitumia dawa za kulevya aina ya heroine.
Manji ambaye alikuwa mshtakiwa alikuwa na mshahidi 7 wakati upande wa mashtaka ulikuwa na mshahidi watatu.
No comments:
Post a Comment