Mahakama Kuu nchini Kenya imeamuru mgombea urais wa chama cha Thirdway
Alliance Ekuru Aukot aliyekuwa ameshiriki uchaguzi mkuu tarehe 8 Agosti
ashirikishwe kwenye uchaguzi mkuu mpya unaopangiwa kufanyika tarehe 26
Oktoba.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi IEBC ilikuwa imetangaza kwamba ni wagombea wawili pekee, Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee na Raila Odinga wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) wangewania kwenye uchaguzi huo.
Bw Odinga alijiondoa kwenye uchaguzi huo Jumanne.
Dkt Aukot amesema amefurahia uamuzi huo na kwamba sasa watakuwa kwenye uchaguzi kwani mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alikuwa amejaribu kuwafungia nje
Hata hivyo, amesema chama chake bado kina masuala ambayo kilitaka yashughulikiwe na tume hiyo ya uchaguzi tangu mwezi Agosti na bado hayajashughulikiwa.
Amesema kukubaliwa kwao kuwania kutawafungulia mlango kufanya mashauriano na viongozi wa IEBC.
Dkt Aukot amesema chama chake kitatoa maelezo ya kina kuhusu msimamo wao katika kipindi cha siku mbili hivi baada ya mashauriano zaidi.
Maafisa wakuu wa IEBC walikutana jana kutafakari kuhusu hatua za kuchukua baada ya hatua ya Bw Odinga lakini kufikia sasa bado hawajatoa tamko.
Kujumuishwa kwa mgombea huyo kuna maana kwamba IEBC haiwezi kumtangaza Bw Kenyatta kuwa mshindi wa moja kwa moja hata baada ya kujiondoa kwa Bw Kenyatta.
Wafuasi wa muungano wa upinzani Nasa wamekuwa wakiandamana Mombasa kushinikiza mageuzi katika tume ya uchaguzi
Ekuru Aukot ni nani?
Dkt Aukot ni mtaalamu wa masuala ya katiba ambaye alikuwa mkurugenzi na afisa mkuu mtendaji wa wa Kamati ya Wataalamu iliyohusika katika kuandika rasimu ya ya Katiba ya Kenya iliyoanza kutekelezwa mwaka 2010.
Alikuwa amesema awali kwamba anataka kuwa rais wa taifa la Kenya kutokana na kile anachosema ni kutoheshimiwa na kuhujumiwa kwa Katiba aliyosaidia kuwepo kwake.
Dkt Aukot alizaliwa miaka 45 iliyopita katika eneo la Kapedo, katika kaunti ya Turkana kaskazini magharibi mwa Kenya.
Alianzisha chama cha Thirdway Alliance katika juhudi za kutoa uongozi mbadala na uongozi wa mageuzi kwa Wakenya.
Anaamini Wakenya hawawezi kuwategemea tena viongozi ambao wamekuwa madarakani kufikia sasa kumaliza ufisadi na ukabila.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na IEBC, Dkt Aukot alipata kura 27,311 sawa na 0.18%, nafasi ya tano kati ya wagombea wanane walioshiriki, katika uchaguzi uliofanyika tarehe 8 August ambao matokeo yake yalifutiliwa mbali na Mahakama ya Juu
No comments:
Post a Comment