MAKALA MAAULUMU YA CHRISTIANO RONALDO ILIOANDIKWA NA SALEHE ALLY - TANZA MEDIA ONLINE

Tuesday, 10 October 2017

MAKALA MAAULUMU YA CHRISTIANO RONALDO ILIOANDIKWA NA SALEHE ALLY




Na Saleh Ally
UTAJIRI wa Cristiano Ronaldo sasa umefikia dola milioni 400 (zaidi ya Sh bilioni 879). Huyu sasa ni mwanamichezo na mfanyabiashara.

Ronaldo anajulikana zaidi kwa kazi yake uwanjani tangu akiwa na Manchester United ya England na sasa Real Madrid ya Hispania na unaweza kusema mafanikio yake makubwa kabisa yamepatikana akiwa na timu mbili tajiri namba moja na mbili duniani.

Wakati Cristiano Ronaldo anakwenda Hispania kujiunga na Real Madrid akitokea Manchester United, wengi waliamini atafeli na ulikuwa mwisho wake kwa kuwa angekutana na mfalme mwingine, Lionel Messi raia wa Argentina ambaye alitua nchini Hispania akiwa na umri wa miaka 13.

Hilo halikumrudisha nyuma Ronaldo ambaye amejiunga na Madrid, leo ni kati ya wachezaji bora zaidi waliowahi kutokea duniani. Kwani amekuwa mchezaji bora wa dunia mara moja akiwa na Manchester (2008), lakini ametwaa tuzo hiyo mara tatu (2013, 2014 na 2016) akiwa na Real Madrid.

Ronaldo anatokea katika Kisiwa cha Madeira nchini Ureno na alizaliwa katika familia ya mtu mwenye kipato cha chini kabisa, José Dinis Aveiro.



Pamoja na kuwa na watoto wanne, Elma, Hugo, Katia na Ronaldo, lakini Aveiro hakuacha kunywa pombe mfululizo hali ambayo kwa kiasi kikubwa ilimkasirisha Ronaldo.

Hata wakati anaanza kupata mafanikio, Ronaldo hakuwa na maelewano mazuri na baba yake kutokana na hali ya ulevi wa kupindukia, leo anajuta, anaamini hakumuelewa baba yake ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 52 baada ya kunywa tena wakati akiwa katika matibabu.

Baba yake, alitamani familia yake iishi katika kiwango cha ndoto zake, lakini mambo hayakuwa kama ambavyo alikuwa akitaka. Jambo lililosababisha muda mwingi kujikuta akitupia ulabu na mwisho ikawa ni tabia yake.

Hivi karibuni, Ronaldo ametamka kwamba anatamani baba yake mzazi angekuwa hai na kumuonyesha alichonacho mkononi kwa kuwa wakati akiwa mdogo alitamani kununua nyumba kubwa na nzuri ya kuishi lakini baba yake alimueleza lisingekuwa jambo rahisi.

“Baba aliingia uoga, mara nyingi nilipomueleza ndoto yangu ya kuwa na nyumba nzuri na gari zuri la kifahari aliniambia niachane na ndoto za mchana.



“Mara nyingi alikuwa akinieleza kuachana na mambo yasiyowezekana. Baba alishakata tamaa, aliona mambo kwake yalikuwa magumu na huenda alihisi ametuangusha,” anasema.

Wakati Ronaldo alikataa kukubaliana na baba yake, aliamua kuwekeza nguvu zake katika kile alichotaka, kile alichoota kukipata na alijua iko siku atafanikiwa ingawa alijua alitakiwa kufanya kazi.

Wako wanaomlaumu kwamba alikosa mazishi ya baba yake. Wakati baba yake alipofariki kutokana na figo zake kushindwa kufanya kazi, Ronaldo ndiyo alikuwa anakwenda uwanjani kuichezea timu ya taifa, alimsisitiza kocha kumpanga na alipata nafasi kidogo ya kulia wakati wa wimbo wa taifa na mwisho alicheza mechi hiyo.

Hajawahi kujibu hilo kwamba hakuelewana na baba yake ndiyo maana alibaki na kucheza lakini yeye ameendelea kuonyesha ana mapenzi na mzee wake lakini amekubali alikosea kutomuelewa na anaona alistahili kumsaidia badala ya kumlaumu kuhusiana na ulevi.


Ukiangalia picha nyingi za Ronaldo wakati akiwa mdogo, utaona yuko na baba yake ambaye alivaa nguo za kiwango cha chini lakini alionekana mtanashati. Aveiro, alijitahidi Ronaldo awe mtanashati zaidi, awe hana tofauti na watoto wa matajiri kwa kuwa hakutaka watoto wake waonekane wanyonge kama alivyokuwa yeye.

Aliishi akitunza bustani na hata kufanya usafi katika baadhi ya barabara. Jambo ambayo lilikuwa mateso makubwa katika moyo wa Aveiro. Je, wewe hadi leo hujamuelewa mzazi wako?

Kama Mwenyezi Mungu amekujaalia kuwa naye hadi leo hata kama ana upungufu unaweza kuanza kumsikiliza leo, kumsaidia na ikiwezekana mpende, mtoe katika sehemu ambayo amekata tamaa na kurejea katika kile unachokiamini sahihi. Sote hatujui Mungu ametupangia kuishi hadi lini. Kama akitangulia kabla yako utajuta.

Kikubwa zaidi, leo ni kuhusiana na yule mwalimu aliyewahi kumuambia maneno Ronaldo ambayo yameendelea kuwa gumzo.


Wakati Ronaldo hajaondoka Madeira kwenda jijini Lisbon kujiunga na akademi ya klabu kubwa ya Sporting Lisbon. Mwalimu wake darasani aliwahi kumtuhumu Ronaldo kuwa ni “kilaza”.

Mwalimu huyo alionyeshwa kukerwa na Ronaldo ambaye alikuwa akizungumzia mpira kila wakati na mwisho akamueleza angekufa masikini kutokana na kuacha kufuata masomo na badala yake kung’ang’ania mambo yake ya mpira.

Mwalimu huyo aliamini mpira ni umasikini na akitaka Ronaldo kujikomboa kwa kujisomea na kufanya vizuri darasani. Jambo ambalo ni kosa kubwa na huenda tayari walimu wengi au wazazi walilifanya.

Vizuri kuheshimu vipaji kama zawadi ya Mungu na kuviendeleza. Kama ni kuhimiza masomo, ziko njia sahihi kuliko kubaki na utamaduni wa kizamani kuamini kucheza soka au kushiriki michezo ni uzembe au ujinga.

Jiulize, Ronaldo angefaulu na kuwa na digrii au ‘Masters’ je, angekuwa na utajiri ambao anao kwa kufanya kazi hospitali? Utajiri alionao wa kuuza mavazi, hoteli anazomiliki na heshima kubwa kama vile kufunguliwa jumba la makumbusho kwa ajili yake na hata jina la Uwanja wa Ndege wa Madeira kupewa jina lake, angevipata?

Walimu wanaokatisha tamaa wengi wenye vipaji hata Tanzania wapo. Wanachoamini ni masomo pekee lakini mtoto anaweza kusoma na kuendeleza kipaji chake kama atapewa muda na kushauriwa vizuri badala ya kushauriwa akiue kabisa kipaji alichonacho.



Ronaldo ana fedha kuliko wote aliosoma nao na wote waliowahi kusoma katika shule aliyosoma tangu ianzishwe. Kweli si kila mmoja anaweza kuwa kama Ronaldo, lakini wako wanaoweza kuishi vizuri na wakapata ajira kupitia michezo na huenda walimu wanapaswa pia kujifunza kuheshimu vipaji na kuvipa nafasi.

Wazazi pia, wanapaswa kujua vipaji ni mtaji mkubwa na haitawezekana katika dunia hii watu wote wakawa na digrii na wenye digrii pekee ndiyo wanaoweza kuwa na mafanikio.

No comments:

Post a Comment