Mfanyabiashara Yusuf Manji ameieleza
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo September 9, 2017 kuwa yeye bado ni
Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu na kudai kuwa hatambui kuvuliwa udiwani
kama ilivyotangazwa na Mstahiki Meya wa Temeke, Abdallah Chaulembo
September 6, 2017.
Manji ametoa malalamiko hayo, kwenye kesi ya uhujumu uchumi
inayomkabili na wenzake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ambapo
katika kesi hiyo ambayo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa
Kishenyi amedai upelelezi haujakamilika na Manji kudai ameona habari
kupitia gazetini kuwa amevuliwa udiwani.
Amedai kama ni kweli amevuliwa Udiwani hatambui, kwani ana miezi 2 yupo gerezani na serikali inatambua kwamba yeye ni Diwani.
”Vikao vya awali vya udiwani wa Halmashauri ya Temeke
nilikuwa nahudhuria kwa kuwa naheshimu Mahakama na kwa uzito wa hii kesi
sikutaka kupeleka hata maombi ya dhamana Mahakamani. Mahakama imuagizie
DPP na aiambie Halmashauri ya Temeke kwamba wamenikamata na ndio sababu
ya kutohudhuria vikao. Kama wanataka nihudhurie DPP aombe remove order
nitolewe gerezani ili niende kwenye vikao.”
Pia Manji amedai kuwa kama hilo haliwezekani, basi wamuandikie barua
itakayoonyesha agenda ya vikao vyote na yeye atazijibu kwa njia ya barua
pia.
”Ninachotambua mimi ni Diwani wa Mbagala Kuu na kama
nimevuliwa au sijavuliwa udiwani sitambui. Tayari nimetumia fedha zangu
mwenyewe zaidi ya Tsh. Milioni 70 sio za Halmashauri kwa ajili maendeleo
ya wananchi wake.”
Aidha, amedai kuwa hiyo kesi ni nzito na DPP hapaswi kuangalia upande
wake wa kesi tu, kwani yeye amechaguliwa na wananchi na anawasaidia.
Awali kabla ya kuelezwa hayo, Wakili wa utetezi Seni Malimi alidai
kuwa wanatarajia kuwasilisha maombi ambayo ni ya siri katika tarehe
ijayo.
Baada ya kuelezwa hayo, Hakimu Huruma Shaidi akautaka upande wa
mashtaka kuhakikisha wanalifanyia kazi suala hilo, ambapo kesi
imeahirishwa hadi September 18, 2017.
SOURCE:MILLARDAYO.COM
No comments:
Post a Comment