Naibu Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabulla ameziagiza
halmashauri zote kuwafikisha mahakani na kuuza mali zao wadaiwa sugu wa
kodi ya pango la ardhi wenye madeni ya muda mrefu.
Dkt. Mabulla
ametoa agizo hilo wakati alipofanya ziara ya kukagua mifumo ya makusanyo
ya kodi ya ardhi mkoani Geita mara baada ya kukuta majina 100 ya
wadaiwa wa kodi ya ardhi ambao hawajalipa kwa zaidi ya miaka 10.
Mhe. Naibu Waziri
wa Ardhi alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Geita
kuhakikisha wadaiwa hao wa muda mrefu wanaandikiwa notisi ya muda wa
siku 14 na wasipolipa ndani ya muda huo wafikishwe mahakamani bila
kuchelewa na kama wasipolipa basi mali zao zipigwe mnada.
Mara baada ya
kubaini hayo Mhe. Mabulla amefanya upekuzi wa nyaraka za umiliki wa
ardhi katika masijala ya ardhi ya Halmashauri ya mji wa Geita na
kugundua uhifadhi mbovu wa hati na ucheleweshwaji utoaji hati za
wamiliki kwa muda mrefu.
Naibu waziri
alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Geita kutembelea mara kwa
mara katika ofisi na masijala za ardhi ili kuhakikisha maafisa wa idara
ya ardhi wanatoa hati kwa wakati na kwa mpangilio mzuri bila kuleta
migogoro.
Aidha, Naibu
Waziri huyo alitembelea eneo lenye viwanja vilivyowekwa mpango wa
matumizi bora ya ardhi katika wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita ambavyo
vimepangwa kujengwa ofisi za serikali, shule, hospitali, makazi, maeneo
ya kuzikia, na huduma nyingine za kijamii.
Naibu Waziri
alimtaka mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale kihakikisha mji huo unapangwa
vizuri na kuwekwa miundombinu ya barabara, maji safi na taka na umeme
ili kuepusha migogoro ya ardhi ambayo mara nyingi huibuka kutokana na
wilaya kutokuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi ya muda mrefu.
Katika hatua
nyingine Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt.
Angeline Mabulla ametembelea eneo la Bombambili mkoani Geita
lililojengwa nyumba 48 za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambapo nyumba
14 tayari zimenunuliwa na Halmashauri ya mji wa Geita.
Mhe. Mabulla
alizitaka halmashauri nyingine nchini kuiga mfano wa halmashauri ya mji
wa Geita kwa kuwashirikisha NHC katika kujenga nyumba bora badala ya
kutumia wakandarasi wa nje wakati Shirika la Nyumba la Taifa lipo na
linajenga nzuri na kwa gharama nafuu.
Naye Meneja wa
NHC Mikoa ya Mwanza, Geita na Simiyu Eng. Benedict Kilimba alimeishukuru
Halmashauri ya mji wa Geita kwa kuwa wakwanza kununua nyumba hizo 14
katika hatua ya awali.
Naibu Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angeline Mabulla anaendelea na
ziara yake ya mikoa ya kanda ya ziwa ambapo anataria kufanya ziara Mkoa
wa Shinyanga hasa katika wilaya ya Kahama na Shinyanga Mjini.
No comments:
Post a Comment