Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe, Dkt. John Pombe Magufuli amesitisha zoezi la bomoa bomoa kwa
Nyumba zaidi ya elfu kumi na saba (17, 000) zilizotangazwa kubomolewa na
Baraza la Hifadhi ya Mazingira NEMC.
Hatua ya kusitisha zoezi hilo, Imekuja
kufuatia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Paul Makonda kuzungumza na
Mhe Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kuhusiana na Sintofahamu ya bomoa
bomoa hiyo ambayo amemueleza Mhe Rais Magufuli kuwa Taarifa za bomoa
bomoa ya Nyumba elfu kumi na saba iliyotolewa haikufika ofisini Kwake
Jambo ambalo ni tofauti na Taratibu za Utendaji kazi wa Serikali.
Mhe Makonda amesema, hata kama
tamko hilo limetolewa na watumishi wa Mkoa mfano Wakurugenzi wa Manispaa
au Wakuu wa Wilaya walioko Chini ya Mamlaka ya Mkuu wa Mkoa
lazima Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ipate taarifa n
iruhusu bomoa bomoa hiyo, na pia hata kama taarifa zimetoka
wizarani inapaswa taratibu za kimaandishi zifuatwe kwa kujulisha Ofisi
ya Mkoa.
“Haiwezekani mtu kutoa tamko la kuvunja nyumba elfu kumi na saba bila mkoa kujua, hilo haliwezekani,” amesema Mhe Makonda.
Makonda amefafanua kuwa ameongea na Mhe
Rais Magufuli na Kumuuliza kama ana taarifa za zoezi la Ubomoaji wa
Nyumba elfu kumi na saba ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Paul
Makonda alimueleza Mhe Rais Magufuli kuwa hana taarifa hizo za ubomoaji,
zaidi Ubomoaji wa Nyumba zilizo kwenye Hifadhi ya Barabara ya kuanzia
Ubungo kwenda Kimara na Mbezi ubomoaji unaofanywa kwa ajili ya upanuzi
wa Barabara ya Morogoro, Ubomoaji wa Nyumba zilizo Jirani na reli
hususani ni zile zinazohusiana na Ujenzi wa Reli Mpya na ya Kisasa.
Kutokana na sababu hizo, Makonda
amesema Rais amesikitishwa na tamko hilo la kutaka kubomolewa kwa nyumba
zaidi ya elfu kumi na saba na ametoa pole kwa wananchi waliokumbwa na
taharuki na tamko hilo la Ubomoaji, na kusisitiza kuwa Rais, Dkt. John
Pombe Magufuli hakuchaguliwa kwa ajili ya kubomoa nyumba za watu na
kusisitiza kuwa anataka wananchi wanaoishi katika maeneo halali kuachwa
maana amepata taarifa kuwa huenda zoezi hilo lingekwenda mbali zaidi
mpaka kwa wananchi wasiohusika.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam Paul Makonda amepiga marufuku zoezi lolote ubomoaji wa
nyumba pasipo ofisi yake kupewa taarifa na kisha kuridhia ubomoaji huo.
Mwisho, Paul Makonda amewataka wananchi
na wakazi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam kuzingatia sheria na wasivamie
maeneo au kuuziwa viwanja na matapeli na pia amewataka wananchi kuchukua
tahadhari hususani ni katika maeneo yote hatarishi ambayo sio
salama kwa wakazi na kuwataka kila mwananchi mwenye familia
kutafuta salama kwa maisha yake na ya familia yake.
Makonda pia ametoa ombi Maalumu Kwa
Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe William Lukuvi la
kuboresha mfumo wa Ardhi katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuanzisha
mpango wa kuweka maafisa ardhi katika kata zote za Mkoa wa Dar es Salaam
ambao watakuwa na jukumu la kusimamia, kuratibu masuala yote ya Ardhi
ngazi ya kata hatua ambayo itasaidia kuondoa Migogoro na utapeli kwa
Wananchi kuuziwa au kununua Ardhi katika maeneo ambayo hayaruhusiwi.
Amesema amepata wazo hilo kutokana na
uzoefu aliopata akiwa Rais wa umoja wa Vyuo Vikuu (TAHILISO) ambapo
alishirikiana na Bodi ya Mikopo kuanzisha mfumo wa kuwa na maafisa
mikopo katika vyuo hatua iliyosababisha kuondoa kero ya wanafunzi
kufuatilia Mikopo katika Ofisi za bodi ya Mikopo hatua ambayo imekuwa
mwarobaini wa tatizo la kufuatilia Mikopo kwa wanafunzi, Mhe Makonda
amesema atamwandikia ombi hilo na kulifikisha Rasmi kwa Mhe Lukuvi ili
amsaidie kulifikisha kwa Mhe Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa ajili
utekekezaji.
No comments:
Post a Comment