Na Saleh Ally
KWA
kipindi hiki hakuna mtu ambaye anaweza kuinua mkono na kusema
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linafanya vizuri sana katika harakati
zake za kuendeleza soka nchini.
Ukiona
mtu anafanya hivyo, basi jua huyo ni shabiki au anataka kuwafurahisha
baadhi ya viongozi wa shirikisho hilo kwa kuwa ni maswahiba wake au naye
anafaidika na kuwepo kwao pale.
TFF
imeboronga hadi imekuwa kero, imekosea mambo mengi sana kwa kuwa mwanzo
wa hesabu zake ulikuwa ni ule wa kukurupuka. Katika viongozi wa
shirikisho hilo, hakuna aliyewaza mipango endelevu, badala yake kila
mmoja alifanya mambo kwa “mpango wa siku”.
Siku
inapokwisha basi kila kitu kimeisha. Huu ndiyo umekuwa ni mwendo wa TFF
na kitu kibaya zaidi ni hiki; hawataki kuambiwa kwa kuwa wanaamini
kuelezwa ni kuhujumiwa.
Hakuna
anayeihujumu TFF, zaidi inajimaliza yenyewe kwa ajili ya matatizo rundo
kama kujaza watu wenye uwezo mdogo kwenye nyanja muhimu kwa kuwa tu ni
maswahiba wa viongozi wa juu.
Tumeona
inaandamwa na matatizo na kashfa kibao, sasa ni nguvu kubwa inatumika
kuzifukia au kuzifunika zisiendelee kusikika wakati zinasikika kila
kukicha.
Tunajua kuhusu uendeshaji wa ligi ulivyo na mapungufu, uwezo mdogo wa waamuzi, ratiba yenye viraka kupindukia.
Imefikia
hata asiyejua mpira anajua kipindi cha TFF chini ya Leodeger Tenga
ambacho kimepita ni bora kuliko hiki cha Jamal Malinzi sasa.
Wadau
wa soka, hata wale waliokuwa wakiutetea uongozi wa sasa au wengi wao,
hawatamani tena na wao ‘wameanza’ kuamini kuwa kweli TFF inaboronga na
inaonekana kushindwa.
Lakini
leo, nina kitu nakubali kuwa tofauti kwamba pamoja na kuinyonga TFF,
kuna jambo tunaweza kuipa kama haki, nalo ni mwendo wa Serengeti Boys
ambayo wamemrudisha Kim Poulsen na hii ni baada ya kukubali kosa kwamba
kuna mtu anayejiita mshauri, alishauri afukuzwe. Wakamlipa mamilioni na
sasa wamemrudisha.
Poulsen
raia wa Denmark anaongoza jahazi la Serengeti Boys akisaidiwa na Bakari
Shime ambaye ni kocha mkuu. Timu inafanya vizuri katika michuano ya
kimataifa na sasa inaonyesha dira, kweli inaweza kuwa mkombozi wa soka
nchini na kuiondoa Taifa Stars hii ya machungu kila mwaka kwa
Watanzania.
TFF
inajitahidi kuonyesha iko tayari kukuza na kuendeleza vijana. Kwa kuwa
imeshindwa kuzisimamia klabu kuwa na timu za vijana, angalau inaonyesha
imepania kuona Serengeti Boys wanafanya vizuri zaidi.
Hadi
sasa, TFF wanastahili pongezi kwa wanavyowalea vijana hao,
wanavyoisimamia kambi yao. Ninaamini fedha kutoka Fifa kwa ajili ya
maendeleo ya soka la vijana zitakuwa zinatumika vizuri ingawa imekuwa
wakijisifia kwamba haina mdhamini na wao wanajitutumua!
Kwanza
kukubali kuigharamia, ni jambo la kupongezwa. Mwendelezo tangu imeanza
hadi sasa, hakika ni jambo jingine la kupongezwa kama watu wanaojali
kabisa.
Ambacho
ninaweza kukumbusha baada ya pongezi hizo, ni TFF kuweka utaratibu
utakaowawezesha vijana hao kuendelea kuwepo. Utakaowafanya wajiendeleze
zaidi kama kupata klabu au vinginevyo.
Kuwa
na utaratibu wa kuwafuatilia badala ya kuwa kama vile enzi zile, baada
ya vijana kumaliza mashindano mfano yale ya Afrika Kusini au Brazil,
basi haijulikani wanafanya nini kipindi hiki maana wengi hawako katika
mpira.
TFF
si klabu lakini bado ina nafasi kubwa ya kuwashikilia vijana
walioonyesha vipaji vya juu na kuhakikisha wanakua kisoka kwa mpangilio
sahihi na baadaye kuja kuwa faida kwa taifa.
Tuliona
Thomas Ulimwengu akikulia katika kituo cha kulea vijana chini ya TFF,
leo ni tegemeo la Tanzania na gumzo la Afrika. Inawezekana kama
wakiamua.
source : http://salehjembe.blogspot.com
No comments:
Post a Comment