MANJI: MKATABA WA TBL ULIKUWA HARAMU YANGA - TANZA MEDIA ONLINE

Sunday 3 July 2016

MANJI: MKATABA WA TBL ULIKUWA HARAMU YANGA

 
 
MWENYEKITI wa Yanga, Yussuf Manji amesema kwamba alilazimika kuuvunja Mkataba wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kutokana na kwamba ulikuwa haramu.
 
Katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari leo, Manji amesema kwamba amevunja Mkataba na huo kuingia Mkataba na Kampuni ya International Marketing ili iitafutie klabu wafadhili wengine wa kuziba pengo la TBL kwa ajili ya mishahara ya Juni. 

"Mkataba wa kampuni ya bia nchini (TBL) na Yanga ulisainiwa miaka mitano iliyopita na mtangulizi wangu.  Huu ulikuwa mkataba haramu, kwani mamlaka ya kutia saini mikataba kwa mujibu wa Katiba ya Yanga yapo kwa wadhamini na hapana kitu kama azimio kutoka  bodi ya wadhamini kuingia katika makubaliano kama haya, au mkataba kusainiwa na wadhamini,"imesema taarifa ya Manji.

Amesema katika kipindi chake kilichopita alijitahidi kurekebisha tofauti zote zilizokuwepo kwenye Mkataba huo, lakini alishindwa.  "TBL ni mara moja tu imetoa Sh. 20 Millioni kwa ajili ya tamasha la Yanga Day zilizoahidiwa kutolewa kila mwaka, haijailipa klabu fedha ya marekebisho inayofikia Sh. 30 Milioni wala haijatupa basi kwa kiwango sahihi tulichotaka kama ililoahidi katika mkataba. 
 
 TBL imejulishwa kuhusu hili lakini haijalishughulikia,"imesema taarifa hiyo. Manji amesema International Marketing ni kampuni ambayo alikuwa Mwenyekiti wake na ikakubali ufadhili huo wa mwezi mmoja, jambo ambalo liliifanya Yanga kuvaa jezi za nembo yake Quality Group katika mchezo dhidi ya TP Mazambe.

"Iwapo wanachama wa Yanga wakihisi nilivunja katiba kwa maslahi yangu binafsi au wakiwa na sehemu nyingine bora zaidi ya kufanya hivyo, walifikishe suala hilo kwenye kamati ya maadili ya klabu kwa ajili ya uamuzi," amesema Manji katika taarifa yake. Manji ameongeza kwamba achaguliwa katika mazingira ya amani zaidi miongoni mwa vyama vya soka nchini na ambapo hakuna hata senti moja ilitumika kwa ajili ya kumhonga yeyote.

"Nilisimama bila kupingwa kugombea nafasi ya Mwenyekiti na nikawaambia wapiga kura wangu waziwazi kwamba: Wakati huu nikiwa Mwenyekiti sitakaa kimya kwa wale watakaojikita katika kuhujumu masuala ya fedha klabuni na wale wanaoamini kwamba TFF iko juu ya sheria zinazohusu masuala ya biashara na haihusiki na Katiba ya Tanzania.  Nawashukuru wapiga kura wangu ambao walinipigia kura kwa asilimia 100 ya ushindi wangu,".

"Masuala yanayotokea uwanjani au usajili wa wachezaji ni ya soka na kwamba TFF ina mamlaka ya  kuipeleka mbele nchi yetu kwa kufuata miongozo ya FIFA.  Lakini sitavumilia upuuzi wa TFF kutaka kuingilia masuala ya Yanga.  Tunajua FIFA imechafuka kwa rushwa na kusababisha Sepp Blatter kuong’olewa na kukabiliwa na mashitaka: hata hivyo, iwapo tungetumia kauli za TFF, Blatter na Platini wasingefanywa chochote,".

"Masuala ya fedha ya klabu yetu, yawe kuhusu nembo ya klabu kwenye kituo cha televisheni bila ya kibali cha Yanga si ya kuamuliwa na TFF.  Kilichopo ni kwamba  kitu cha televisheni kinatengeneza fedha kutoka kwa Yanga, TFF inatengeneza fedha kutoka kituo cha televisheni.  Hivyo, iwapo kuna mtu anafikiri sijui sheria za mashindano  bora ya kibiashara na hakimiliki, basi wajue hilo litawagharimu,".

"Iwapo TFF inataka Mwenyekiti wa Yanga akubaliane na uwongo, basi katika miaka minne ijayo niko tayari kupambana na uovu huo na kusahihisha kila kitu.    Hata hivyo, kwanza kabisa niko tayari  kushirikiana kirafiki  na wakati huohuo kupigania haki za klabu kwani daima nimekuwa mtu mwenye kupigania haki na masuala ya kikanuni ninayoyaamini ni ya kiadilifu,".

"Yanga ilikuwepo kabla yangu na itakuwapo baada yangu.  Ni wajibu wangu kuiacha Yanga ikiwa klabu bora zaidi kuliko nilivyoikuta na nikiona siwezi tena kutumikia maslahi ya wanachama wake, sitasita kujiuzulu au kuitisha uchaguzi ili kujipanga upya,".

No comments:

Post a Comment