THAMANI YA THABAN KAMUSOKO NI SAWA NA VIUNGO WATATU WA SIMBA SC’ - TANZA MEDIA ONLINE

Wednesday, 24 February 2016

THAMANI YA THABAN KAMUSOKO NI SAWA NA VIUNGO WATATU WA SIMBA SC’

Mwinyi Kazimoto 2

Ikijiandaa na mchezo wake wa kombe la FA siku ya Jumatano hii dhidi ya JKT Mlale ya Ruvu, timu bingwa-mtetezi na vinara wa ligi kuu Bara, Yanga SC imewataka mahasimu wao wa soka nchini kuacha kulalamikia uamuzi wa mchezo wao wa Jumamosi iliyopita ambao Simba SC ilichapwa 2-0 na badala yake waelekeze akili yao katika kujadili na kutafutia ufumbuzi wa makosa yao ambayo yamepelekea kuchapwa katika michezo yote miwili waliyokutana msimu huu.
“Kama mwalimu (kocha) anayejua mpira ambaye amefungwa hajafungua mdomo wake kumlalamikia mwamuzi, na wala hakuwa na ujasiri wa kumlalamikia, sasa inakuwaje mtu ambaye hajasoma hata ‘vidudu’ (ngazi ya kwanza ya elimu ya awali kwa mtoto) wanakuwa na ujasiri wa kulalamika. Wanapata wapi ujasiri wa kumlalamikia mwamuzi.” anasema Jerry Muro, afisa mkuu wa kitengo cha habari katika timu hiyo.
Baadhi ya viongozi, wanachama na mashabiki wa Simba wamekuwa wakilalamikia uchezeshaji wa mwamuzi, Jonesia Rukyaa ambaye alimuondoa uwanjani kwa kadi mbili za njano mlinzi wa Simba, Abdi Banda.
“Kama mnakumbuka mwamuzi huyu (Jonesia) aliwahi kumwonyesha kadi nyekundu nchezaji wetu katika mchezo wa Mtani Jembe (2014) lakini sisi kama viongozi hatukulalamika, tulikubali matokeo na tukaondoka”, anasema zaidi Muro akikumbushia tukio mlinzi wao Kelvin Yondani kutolewa uwanjani katika mchezo wa Mtani Jembe-2.
“Katika sheria 17 za soka unapomkwatua mchezaji akiwa mbele yako, wewe uko nyuma, lazima upewe adhabu, na adhabu ambayo inatajwa kule ni kadi ya njano kulingana na mazingira au mwamuzi anaweza kutoa adhabu ya juu zaidi, kwa hiyo sisi hatukumtuma yule mchezaji (Banda) amkwatue mchezaji wetu (Ngoma.)”
Muro aliwapiga dongo Simba kwa kuwaambia kwamba thamani ya kiungo wao Thaban Kamusoko katika mechi hiyo inalingana na viungo watatu wa Simba.
“Lakini pia tuwakumbushe wapinzani wetu kuwa thamani ya mchezaji wetu mmoja wa nafasi ya kiungo ni sawa na kuchanganya viungo wao wote watatu. Ukiwachanganya viungo watatu wa Simba ndio unapata thamani ya Kamusoko. Kwa hiyo wasiweke sababu nyingine. Jamani mbona rahisi tu, tumewala mara ya kwanza 2-0, na safari hii 2-0 sasa mtasema tumepatia au tumeotea.”

No comments:

Post a Comment