MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Hussein Nyika, amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kusema mshambuliaji wao, Obrey Chirwa haendi popote, anabaki Jangwani na tayari wameanza kumuandalia mkataba mpya.
Nyika ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tangu ziwepo tetesi za Simba kufanya mazungumzo na Chirwa kwa ajili ya kusaini mkataba wa kuichezea timu hiyo kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Chirwa hivi sasa anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine itakayomhitaji kwa ajili ya kusaini mkataba kwa mujibu wa kanuni kwani amebakisha miezi sita katika mkataba wake.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Nyika alisema hawana mpango wa kumuachia Chirwa na kwenda timu nyingine kutokana na umuhimu na mchango wake katika timu.
Nyika alisema, wapo katika mazungumzo na Chirwa kwa ajili kumuongezea mkataba mpya wa kuichezea timu hiyo na kila kitu kitakamilika kabla ya ligi kumalizika.
“Niwaondoe hofu mashabiki wa Yanga kwa kuwaambia kuwa, mipango yote ya kumbakisha Chirwa inakwenda vizuri kwa maana ya kumpa mkataba mpya.
“Kwanza Chirwa bado mchezaji wetu halali mwenye mkataba unaotarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, ni vyema hao wanaosambaza taarifa hizo wakalifahamu hilo.
“Tupo katika hatua nzuri ya kumalizana na Chirwa ambaye tunaamini msimu ujao tutakuwa naye kwa ajili ya kuichezea timu yetu,” alisema Nyika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano.
Nyika alisema tofauti na Chirwa, wapo kwenye mazungumzo na wachezaji wengine wanaomaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu ili kuhakikisha wanakiimarisha kikosi chao.
No comments:
Post a Comment