DAR ES SALAAM: Wakati Wabongo Baraka Malali na mkewe, Ashura Mussa wakazi wa Magomeni jijini Dar wakisubiri hukumu ya kesi yao baada ya kunaswa na madawa ya kulevya Guanzhou nchini China, serikali imewatolea tamko Watanzania, Jack Cliff maarufu Jack Patrick na Video Queen, Sandra Khanmaarufu Binti Kiziwi ambao walinaswa na dawa za kulevya nchini humo tangu mwaka 2013.
Mke na mume huyo walinaswa na madawa ya kulevya jumla ya pipi 129 tumboni ambapo kwa mujibu wa sheria za Guanzhou, serikali ilisema wawili hao hawatakwepa adhabu ya kunyongwa wakikutwa na hatia, tukio ambalo liliibua mjadala kwa Watanzania Jack Patrick na Binti Kiziwi ambao nao walikamatwa nchini humo miaka mitano iliyopita na mpaka sasa kimya kimezidi kutanda.
Kufuatia tukio hilo kumekuwa na maneno mengi kuhusu mastaa hao huku wengi wakisema kuwa wameshanyongwa na wengine wakisema wamefungwa maisha huku wachache wakisema wanatarajia kumaliza vifungo vyao hivi karibuni.
Ili kupata ukweli kuhusu sheria za China kuhusiana na wanaokamatwa na madawa ya kulevya, Jumatatu iliyopita mwandishi wa Gazeti la Amani alikwenda Mamlaka ya Udhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya (DCEA), iliyopo Posta jijini Dar na kufanya mazungumzo na Kamishna wa Sheria wa Mamlaka hiyo, Edwin Kakolaki na kuulizia hatima ya Wabongo hao.
Mwanahabari wetu alianza kuulizia kuhusu hatima ya Jack Patrick aliyekamatwa Kisiwa cha Macau nchini China Desemba 19, mwaka 2013 akiwa na madawa ya kulevya aina ya heroin yenye uzito wa kilo 1.1 ambapo Kamishna Kakolaki alifafanua suala hilo kwa kusema kuwa kisiwa hicho ni sehemu ya China kiutawala lakini kiuchumi na kisheria kinajitegemea.
Alisema kuwa Macau ni eneo ambalo unaweza kulifananisha kama ilivyo Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuwa hata Bunge, wanalo la kwao ambalo linajitegemea.
“Wao sheria zao kuhusu madawa ya kulevya zilifanyiwa marekebisho mwaka 1996, na unapokamatwa na kiwango cha kuanzia kilo moja adhabu yake ni kifungo jela cha kati ya miaka mitano mpaka kumi na tano ingawa sina uhakika na miaka aliyohukumiwa Jack Patrick,” alisema.
Kamishna huyo aliongeza kuwa kama hiyo ni mara yake ya kwanza kunaswa nchini humo, atapewa adhabu ndogo ambayo ni hiyo miaka mitano lakini kama atakuwa amerudia au kunaswa na kiwango kikubwa zaidi ndipo anaweza kufungwa mpaka hiyo miaka kumi na tano na hakuna faini.
Kutokana na ufafanuzi huo na kwa kuwa mrembo huyo alikamatwa Desemba 19 mwaka 2013 na kuhukumiwa wiki hiyohiyo hivyo tarehe kama hiyo mwaka huu ndiyo atakuwa amekaribia kutimiza miaka mitano jela na huenda baada ya hapo akaachiwa huru.
Akimzungumzia Binti Kiziwi, aliyenaswa Hong Kong, Julai 15 mwaka 2013 na madawa ya kulevya aina ya heroin zaidi ya kilo moja na kuhukumiwa wiki hiyohiyo, Kamishna Kakolaki alisema unapokamatwa na madawa ya kulevya kuanzia kilo moja adhabu yake ni kifungo cha maisha au faini ya shilingi bilioni 1.4 (kwa pesa za Kitanzania).
“Hivyo, ili Binti Kiziwi aachiwe gerezani, inabidi atoe kiasi hicho cha fedha aidha kwa kuchangiwa au vyovyote, vinginevyo na kwa sheria za Hong Kong kwa kuwa hakutoa fedha, tayari ameshafungwa maisha.
“Kikitolewa kiasi hicho cha fedha anaachiwa huru hata kesho,” alisema Kamishna Kakolaki.
Aliendelea kuichambua Hong Kong na kusema mji huo unapokutwa unatumia madawa hayo kwa kuvuta, kujidunga au vyovyote vile, utakabiliwa na adhabu ya kifungo cha miaka saba jela au faini ya Shilingi milioni 287 kwa thamani ya pesa ya Kitanzania.
Akiwaelezea mke na mume waliokamatwa Guanzhou nchini humo hivi karibuni, alisema hao waombewe wasipatikane na hatia lakini kama wakipatikana na hatia kwa mji huo hukumu yake ni kunyongwa tu hakuna nyingine.
Akizungumzia suala la kuwatetea Wabongo hao Kamishna Kakolaki alisema nafasi bado ipo kwani wanaruhusiwa kuweka mawakili kama washitakiwa wengine.
“Kama wanataka kuweka mawakili wazuri wa kuwatetea nafasi hiyo bado ipo ingawa si kazi ndogo.
“Tulipowasiliana na vyombo vya usalama vya huko China walisema watatujulisha kila hatua ikiwemo matokeo ya hukumu.
“Hivyo kama wana mawakili kutoka hapa nchini au wakitaka wa hukohuko China nalo pia linawezekana, ni wao tu, “ alisema Kamishna Kakolaki.
Hata hivyo, alitoa onyo kwa watumiaji, wauzaji na wasafirishaji wa madawa hayo kuwa kujihusisha na madawa hayo haramu ni jambo hatari na endapo watakutwa na hatia adhabu zake huwa hazina msamaha.
Stori: Richard Bukos, Gazeti la Amani
No comments:
Post a Comment