Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amefanya mabadiliko ya kamati mbalimbali za kudumu za bunge kwa mujibu wa Ibara ya 96 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Taarifa iliyotolewa na bunge imesema kuwa ibara hiyo ya 96, imelipa uhalali Bunge la Jamuhuri ya Muungano Tanzania kuunda kamati za Bunge za namna mbalimbali kadri itakavyoona inafaa kwa ajili ya utekelezaji bora wa madaraka yake.
Aidha ibara hiyo imeweka wazi kwamba kanuni za kudumu za Bunge zitafafanua muundo wa shughuli za kamati za Bunge.
Kanuni ya 118 ya kanuni za kudumu za Bunge, toleo la Januari 2016 imeweka kamati za kudumu za Bunge zenye muundo wa majukumu mbalimbali kama yanavyofafanuliwa kwenye nyongeza ya nne.
Kamati hizo zimetekeleza majukumu yake mpaka tarehe 9 Februari , 2018 ambapo ni mwisho wa mkutano wa kumi wa Bunge ambao unakamilisha nusu ya uhai wa Bunge la kumi na moja. Hivyo kwa mujibu wa kanuni ya 116(7), kipindi hicho ndio ukomo wa ujumbe katika kamati walizokua wakizifanyia kazi wabunge.
Hata hivyo, kwa mamlaka aliyopewa Spika na kanuni ya 116(3) na kwa kuzingatia vigezo vilivyoainishwa katika kanuni ya 116(5) amefanya uteuzi mpya wa wajumbe katika kamati za kudumu za Bunge na wajumbe wa kila kamati ya kudumu wanawajibika kuchagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti kwa mujibu wa kanuni ya 116(10) kuwa viongozi wao.
No comments:
Post a Comment