Mshauri mwandamizi wa uchumi wa rais Donald Trump, Gary Cohn amejiuzulu wadhifa wake, na kumfanya kuwa afisa wa karibuni katika mfululizo wa maafisa wa ngazi ya juu wanaoachia ngazi katika utawala wa Marekani, mwingine ni akiwa aliyekuwa msiri wa kuaminika zaidi na Trump, Mkurugenzi wa Mawasiliano Hope Hicks na wengine.
Vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kwamba Cohn, Mdemokrat na anayepigia upatu biashara huria, amekuwa akiongoza wale wanaopinga ndani ya nchi mpango mzima wa Rais Donald Trump wa kuweka ushuru katika uingizaji wa chuma na aluminium.
Trump amekaidi mtazamo huo, na kusisitiza kuwa ataanzisha ushuru huo katika siku chache zijazo.Trump kupitia ukurasa wake wa Twitter ameandika kwamba “atafanya maamuzi hivi karibuni ya kumteua mshauri mpya wa uchumi.Zaidi Trump amesema wapo watu ambao wangependa kufanya kazi Ikulu.
“Watu wengi wanataka kuingia. Ninaweza kuchagua yeyote. Ninaweza kuchukua nafasi yoyote White House na nitachagua watu 10 bora wanaohusika na nafasi hiyo. Kila mtu anataka kuja hapa na wanaipenda White House kwasababu tuna nguvu kuliko hapo kabla.” amesema Trump
Aidha, Mkuu wa utumishi John Kelly amesema Trump amemshukuru Bw. Cohn kwa utumishi wake, na kumuelezea kama mmoja ya watu wachache walio na “vipaji”, na kwamba ameitumikia nchi yake kwa utumishi uliotokuka.