Mwenyekiti wa Chama cha UDP, John Cheyo amesema kuwa maandamano na mikutano ya hadhara sio njia ya kuondoa kero za wananchi pamoja na viongozi wa upinzani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Cheyo amesema kuwa maandamano yanayohamasishwa kupitia mitandao ya kijamii kufanyika Aprili 26 sio hatua sahihi na kuwataka Watanzania kulinda amani iliyopo.
“Tusikae tukafikia hatua ya kuandamana barabarani tukidai haki, Katiba Mpya, Tume huru ya uchaguzi. Tukifikia huko, amani iliyopo Tanzania tutashindwa kuipata tena na wananchi watakosa nchi nyingine yenye amani ya kuikimbilia,” alisema Cheyo ambaye aliwahi kugombea urais.
Aliongeza kuwa haungi mkono madai ya mikutano ya hadhara hata kama inadaiwa kwa lengo la kuongeza wanachama kwani anaamini mitandao ya kijamii hivi sasa ina nguvu na inaweza kutumika.
Amesema njia bora inayopaswa kutumiwa na wanasiasa nchini ni kutumia mabaraza ya vyama vya siasa, na kwamba Rais John Magufuli anapaswa kutoa fedha kuwezesha mabaraza hayo.
Akitoa mfano wa mikutano ya kampeni ya chaguzi ndogo zilizofanyika hivi karibuni, alisema kuwa mikutano ya hadhara ilitawaliwa na matusi na hata maandamano yaliyofanyika yalisababisha kifo cha mwanafunzi asiye na hatia.
“Siungi mkono hoja ya kudai mikutano ya hadhara hata kama ni kwa lengo la kuongeza wanachama kama wanavyodai wengine. Naamini kwa sasa mitandao ya kijamii ina nguvu kuliko kitu chochote nchini,” alisema.
Aidha, aliwataka viongozi wa dini kuwa kiunganishi kati ya wananchi na viongozi wa kisiasa na sio vinginevyo