MBUNGE wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu kama ‘Sugu’
na mratibu wa chama hicho Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel
Masonga wameitwa katika Kituo Kikuu cha Polisi mkoani humo huku wakisema
hawajui sababu ya wito huo.
Wawili hao wamesema wanahisi wito huo unatokana na mkutano wa hadhara
alioitisha mbunge huyo katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini
Mbeya.
Sugu amesema leo Jumanne kuwa, juzi jioni alipigiwa simu na Mkuu wa
Upelelezi Mkoa wa Mbeya (RCO) kwamba yeye na Masonga wafike jana ofisini
kwa ajili ya mazungumzo lakini alimueleza kuwa itakuwa ni siku ya
sikukuu hivyo itakuwa vigumu ngumu kwenda, hivyo walikubaliana wafike
leo.
“Polisi walinipigia simu juzi jioni wakinitaka mimi na Masonga twende
Makao Makuu ya Polisi jana, nikawaambia itakuwa ni sikukuu hivyo
tukakubaliana leo asubuhi. Sasa hivi tupo njiani tunaelekea huko kuitika
wito. Sijajua sababu, lakini nadhani ni uchochezi,” amesema Sugu.
Masonga amesema anaamini sababu ya kuitwa kwao inatokana na mkutano
wao wa hivi karibuni na wananchi ambapo Masonga ndiye aliyemkaribisha
Sugu kuzungumza na wananchi na alifunga mkutano, lakini kabla ya
kumkaribisha alizungumza machache.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga hajazungumzia wito huo.
No comments:
Post a Comment