Kiongozi wa kikundi
cha wapiganaji wa Boko Haram Abubakar Shekau, ameonekana kwenye video
mpya karibu saa ishirini na nne baada ya Rais wa Nigeria Muhammadu
Buhari kwa mara ingine kutamka hadharani kuwa kikundi hicho
kimesambaratishwa.
Huu ni mkanda wa video wa kwanza kutolewa na
Shekau baada ya kimya cha miezi kadhaa iliyopita, naye ni mongoni mwa
viongozi wanaosakwa kwa hamu na ghamu na kupewa sifa ya kuwa miongoni
mwa magaidi wanaosakwa na Marekani pamoja na mamlaka ya Nigeria.
Abubakar
Shekau anaonekana kwenye mkanda huo wa video akiwa ameketi peke yake
akiwa amevalia kanzu,kofia yenye rangi inayofanana na bunduki aina ya
AK-47 ambayo anaonekana kuwa na mahaba nayo.Lakini anaonekana kushindwa
kuzungumza kwa sauti yenye mamlaka ikilinganishwa na matamko yake ya
awali .
Akisoma kutoka katika karatasi kwa lugha ya kiarabu na ki
Hausa, Shekau, anakiri kundi lake kuhusika katika matukio ya hivi
karibuni nchini Nigeria katika maeneo ya kaskazini-mashariki mwa nchi
hiyo ikiwemo lile lililotukia siku ya siku kuu ya Christimas katika
kijiji cha Molai nje ya jiji la Maiduguri, mji mkuu wa Jimbo la Borno.
Shekau
alijinasibu kwa kusema kuwa askari wa kundi la wanamgambo la Boko Haram
wana afya maridhawa na kwamba vikosi vya ulinzi nchini Nigeria
haviwezi kufanya lolote dhidi ya wanamgambo wake.
Sehemu ya dakika thelathini na moja ya mkanda huo zimeoneshwa
mbwembwe za wapiganaji wa kundi hilo ikiwemo magari ya silaha, malori na
pikipiki huku wakinapiga risasi hewani kwa kile kinachoonekana kizuizi
cha njiani katika kambi ya kijeshi iliyotelekezwa .
Wakati huo
huo Shekau alionekana akitoa tamko juu ya kukerwa kwake dhahiri juu ya
kutambuliwa hivi karibuni mji wa Yerusalemu kama mji mkuu wa Israeli
tamko lililotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump, Abubakar Shekau,
ameijosoa nchi ya Saudi Arabia kwa kushirikiana na wale aliowaita
makafiri na kuwalaumu Wapalestini kwa uharibifu wao.
Mpaka sasa
serikali ya Nigeria haijatoa tamko lolote juu ya mkanda huo wa video na
ujumbe uliomo ndani yake. Hata hivyo jeshi la Nigeria linakiri
kuwafukuza waasi kutoka katika ngome zao kaskazini-mashariki mwa nchi
hiyo, hata hivyo wanamgambo wa kikundi cha wapinaji cha Boko Haram
bado wanaendeleza mashambulizi ya kujitoa muhanga , mashambulizi ya
risasi za moto zaidi wakilenga vifaa vya kijeshi na vijiji.
No comments:
Post a Comment