Tundu Lissu akiwa ameketi.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu (Chadema) leo amekaa mwenyewe pasipo msaada wa madaktari katika
Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, anakotibiwa baada ya kushambuliwa kwa
risasi nyumbani kwake, Area D, Dodoma huku hali yake ikizidi kuimarika
kila kukicha.
Desemba 26, mbunge huyo alisimama kwa
mara ya kwanza na kuanza rasmi kufanya mazoezi ya viungo katika
Hospitali hiyo kwa msaada wa madaktari. Lissu anaendelea na mazoezi
madogo ya kuimarisha misuli ya miguuni ili aweze kutembea.
Akielezea hali yake, Mhe. Tundu Lissu
amesema kwa sasa anauwezo wa kukaa bila kuegemea kwenye kitu chochote,
hali ambayo awali alikuwa anashindwa kufanya hivyo.
“Ninawashukuru kwa sala na maombi yenu. Sasa ninaweza kukaa bila ya kuegemea kitu.“ameandika Mhe. Lissu kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Mwanasheria mkuu huyo wa Chadema,
ambaye alishambuliwa kwa risasi akiwa ndani ya gari mara baada ya kufika
nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 7, hivi karibuni alisema bado
ana risasi moja mwilini mwake ambayo haijatolewa.



No comments:
Post a Comment