DAR ES SALAAM: Ikiwa
ni takriban siku sita tangu mlimbwende maarufu Bongo, Wema Sepetu
ang’atuke Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Jonathan Lema ameibuka na kuzungumza mambo yaliyokuwa
nyuma ya pazia kumhusu mrembo huyo.
Wema alitangaza uamuzi wake wa kukihama
Chadema na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM), Ijumaa iliyopita
kupitia ukurasa wake wa Instagram.
CHANZO CHAVUJISHA
Awali, chanzo makini kilicho ndani ya
Chadema, kilieleza kuwa, miezi michache baada ya Wema kujiunga na chama
hicho, ilibainika ni mchanga sana kisiasa tofauti na walivyotarajia.
KUMBE WALIJUA WEMA ‘MWANAFUNZI’
Kilisema baada ya kubainika hivyo,
Chadema walijua kabisa kuwa anaweza kubadilika wakati wowote hivyo
waliona anahitaji kupewa darasa la kisiasa ili aweze kuwa imara. Chanzo
hicho kilienda mbele zaidi kwa kusema, ililazimika baadhi ya viongozi
wazoefu wa chama hicho kuchukua jukumu la kumkuza kisiasa.
ALIANZA KUKUZWA KISIASA
“Viongozi mbalimbali tu wakaanza kumpa
darasa. Waligundua alipokuwa CCM hakuwa anaijua siasa wala kuwa na ule
ujasiri wa kuwa mpinzani, wakaanza kumjenga,” kilidai chanzo hicho.
Kilipobanwa zaidi chanzo hicho ili
kiweze kuwaweka bayana viongozi hao ambao walijitolea kumfundisha mrembo
huyo ndipo aliposema ni viongozi tofauti, akiwemo mbunge wa Arusha,
Lema.
“Ni viongozi wengi tu ambao wengi wao
walikuwa ni wa ngazi ya chini lakini kwa ngazi za juu, Mbunge wa Arusha
Mjini (Lema) kipindi kile alipokwenda kumtambulisha kwa mara ya kwanza
jimboni kwake,” kilizidi kudai chanzo hicho.
HUYU HAPA LEMA
Amani lilimtafuta Lema kupitia simu
yake ya mkononi ambapo awali, aliomba asimzungumzie mrembo huyo kwani
hana umuhimu wowote mkubwa ndani ya chama.
Mwanahabari wetu alipozidi kumuomba
tena na tena amzungumzie japo kwa yale ambayo tayari chanzo makini
kilikuwa kimeshalieleza Amani, Lema akafunguka ambayo watu hawajui
kuhusu Wema:
“Huyo (Wema) hakuna sababu ya
kumzungumzia sana. Kwanza kama watu wanafikiri alikuja akiwa anaijua
siasa na pengine ni faida kwetu waelewe si kweli. Alikuwa mtupu sana.
Kwa hiyo kuchukua muda wangu kumuongelea ni kumpa popularity (umaarufu)
asiostahili kabisa na ninyi wanahabari mtusaidie kuepuka haya mambo.”
ATHIBITISHA KUFUNDISHWA
“Alikuja kufundishwa siasa. Hakuwa
akijua chochote. Mimi nafikiri tusipoteze muda sana kumjadili maana hata
katika mafunzo tulijua kwamba anaweza kubadilika na kweli amebadilika,”
alisema Lema.
AANIKA JINSI MKEWE ALIVYOMNOA
Akizidi kushusha dondoo za mrembo huyo,
Lema aliweka bayana kuwa kuna mambo mengi ambayo watu hawayajui kuhusu
namna mrembo huyo alivyokuwa anafundwa na mkewe.
“Naweza kukutumia video fupi (clip) ya
mke wangu Neema uone namna ambavyo alikuwa akimfundisha na kumuongoza
kwa mambo mengi ya kisiasa na maisha kwa ujumla (hakutuma video
yenyewe), muhimu ndugu yangu (akilitaja jina la mwandishi wetu)
tusaidiane kukuza demokrasia na siyo kupoteza muda kwa mambo yasiyokuwa
na tija kama hayo.
“Katika maisha kuna watumwa wa aina
tatu, kuna watumwa wanakula keki, kuna watumwa wanakula mkate na kuna
watumwa wanakula mihogo mibichi, wote hao ni watumwa,” alisema Lema bila
kufafanua maana ya mfano huo na kuongeza;
“Sema wakati tunategemea anaweza
kuelekea kuzuri na akiwa hajaiva vilivyo, huyooo akahama. Tumuache tu
bwana hakuna hata sababu ya kutumia nguvu nyingi kumzungumzia mtu
ambaye ndio kwanza ni mwanafunzi na hana uzito wa kushtua kama ambavyo
watu wanataka kutengeneza,” alisema Lema.
MBOWE VIPI?
Amani lilimtafuta Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Aikaeli Mbowe ili kumsikia anamzungumziaje mrembo huyo
ambaye wengi waliamini alikuwa na mchango katika chama hicho, lakini
alipopatikana alimpuuza na kuomba aulizwe mambo ya msingi ya kitaifa.
“Huyo mimi siwezi kumzungumzia. Kama una jambo la kitaifa unaweza kuniulizia lakini kwa huyo achana naye,” alisema Mbowe.
TUMEFIKAJE HAPA
Februari mwaka huu, Wema na mama yake
ambao walikuwa wafuasi waaminifu wa CCM, walitangaza kung’atuka katika
chama hicho na kujiunga na Chadema kwa kile walichodai kwenda kuifanya
demokrasia ya kweli.
Uamuzi huo waliufanya ikiwa ni siku
chache baada ya mrembo huyo aliyeipigia CCM kampeni katika uchaguzi wa
mwaka 2015 atajwe kwenye orodha ya wasanii wanaojihusisha na masuala ya
madawa ya kulevya.
Kupitia sakata hilo, Wema hadi sasa anakabiliwa na kesi ya madawa ya kulevya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
chanzo: globalpublishersonline.com
No comments:
Post a Comment