Jeshi la Israel limefyatua makombora kadhaa kuelekea eneo la Gaza, Palestina ikilenga wapiganaji wa kundi la Hamas.
Jeshi hilo la Israel limeeleza kuwa katika mashambulizi hayo lilipiga
maeneo ya viwanda vya uzalishaji wa silaha na maghala ya silaha ya
Hamas, mapema leo. Hata hivyo, kwa mujibu wa Independent, makombora hayo
yalileta madhara katika maeneo ya makazi yakigusa pia watoto.
Hamaki kati ya Israel na Palestina iliongezeka wiki iliyopita baada ya
Rais wa Marekani, Donald Trump kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa
Israel.
Israel imekuwa ikidai Jerusalem ni mji wake mkuu wakati Wapalestina
wakiendelea kudai upande wa Mashariki mwa mji huo kuwa eneo lao muhimu
lililotwaliwa na Israel katika vita ya mwaka 1967.
Jana, kiongozi wa Hamas, Fathi Hammad alisema kuwa Taifa lolote
litakalohamishia ubalozi wake Jerusalem litakuwa ‘adui wa Wapalestina’.
Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Nje, Augustine Maige imeweka wazi
msimamo wake kuwa haitahamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv kwenda
Jerusalem.
“Hatuna ulazima wa kuhamisha ubalozi wetu. Unapaswa kufahamu kuwa
ubalozi wa Tanzania nchini Israel utabaki kuwa Tel Aviv na hakuna mpango
wa kuuhamishia Jerusalem ingawa kumekuwa na jitihada za kutushawishi
kufanya hivyo,” Waziri Maige anakaririwa na The Citizen.
Uamuzi wa Trump umepokelewa kwa hisia tofauti na mataifa mengi huku
ikielezwa wazi kuwa utakwamisha mazungumzo ya amani kati ya Israel na
Palestina.
No comments:
Post a Comment