Dk. Salim Ahmed Salim atoa mtazamo wake mgogoro wa Palestina na Israel - TANZA MEDIA ONLINE

Friday, 8 December 2017

Dk. Salim Ahmed Salim atoa mtazamo wake mgogoro wa Palestina na Israel



Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Dk. Salim Ahmed Salim amefanya mazungumzo na Kamati ya Umoja wa Mataifa (UN) inayotetea haki za msingi za Wapalestina katika mgogoro wao na taifa la Israel.

Dk Salim aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), katika mazungumzo yake na wajumbe hao amesisitiza umuhimu wa kufikiwa suluhu kwa mgogoro huo ili watu wa Palestina wapate haki zao za msingi.

Alisema kuna kila sababu ya pande zote kuheshimu maadhimio ya UN katika kufikia suluhu juu ya mgogoro huo, akizungumzia wazo la Israel kuufanya Jerusalem kuwa mji mkuu wake, alisema hali ni ngumu kwa Waparestina na Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa limepitisha maadhimio mengu juu ya mgogoro huo lakini yamekuwa yakipuuzwa na Serikali ya Israel hivyo kuishauri kuyazingatia.

Aliipongeza Kamati ya Umoja wa Mataifa (UN) inayotetea haki za msingi za Wapalestina kwa juhudi zake za kutafuta suluhu ya mgogoro huo na kuitaka jamii ya kimataifa kuunga mkono juhudi za kamati hiyo ili ifikie malengo yake.

Tayari viongozi wa Wapalestina wamelaani hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel na kusema hatua hiyo ni kufifisha juhudi za kutafuta amani Mashariki ya Kati.

Kamati ya Umoja wa Mataifa (UN) inayotetea haki za msingi za Wapalestina mara baada ya mazungumzo na Dk. Salim Ahmed Salim walimkabidhi kitabu cha picha za historia ya Waparestina na mgogoro huo.

Hata hivyo, Kamati ya Umoja wa Mataifa (UN) inayotetea haki za msingi za Wapalestina inatarajiwa kukutana na kujadiliana juu ya hatua ya Israel kutaka kuutangaza mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wake.

No comments:

Post a Comment