BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
kimeitaka Serikali kuunda tume huru kwa ajili ya kuchunguza matukio ya
uvunjifu wa amani yanayotokea nchini.
Baraza hilo limesema kwamba Rais John Magufuli anapaswa kuunda tume
hizo huru za kiuchunguzi zikiwahusisha watu kutoka nje ya nchi ili
kusiwepo na kigugumizi wala upendeleo katika kufanya kazi hiyo.
Mwenyekiti wa baraza hilo Patrobas Katambi amesema hayo leo Septemba
9 kwamba tume hiyo ambayo itakuwa na kazi ya kuwachunguza watu
wasiojulikana inapaswa kukihusisha chama chao kwa sababu viongozi wao
wengi wamekumbwa na vitendo hivyo.
“Yamekuwa yakitokea mauaji, kutishiana silaha, utekaji na kujeruhi
lakini vyombo vya dola vimekuwa vikisema wanaofanya hivyo ni watu
wasiojulikana. Jambo ambalo linaashiria watu hao wanaizidi nguvu
Serikali,” anasema Katambi.
“Ni muhimu kuchukua hatua hiyo kwani watu hao wasiofahamika wanaweza kumdhuru yeyote hata Rais wa nchi au yeyote mwenye damu” anasema Katambi.
Anasema vijana wa Bavicha wapo tayari kushirikiana Polisi masaa 24 na
siku 360 ili kuwabaini watu hao wasiofahamika ambao wamekuwa tishio kwa
usalama wa nchi.
“Hakuna mtu aliyewahi kufanya uhalifu duniani kote na asifahamike ni
hapa tu kwetu kila tukio tunaambiwa wahusika hawajafahamika. Bora hata
itumike picha ya Setilite lakini mtuhumiwa apatikane nadhani hapa
kinachokosekana ni utashi tu,” anasema.
Kuhusu suala ka kupigwa risasi kwa kada wa chama hicho Tundu Lissu
Katambi anasema vyombo vya dola bado vinafanya kazi yake lakini wao
wanaweza kufanya na kudadavua tu mazingira ya tukio hilo na kujua
wahusika.
“Nimewahi kulala kwa Lissu pale Dodoma kipindi nina kesi katika mji
ule, nyumba yake iko jirani na nyumba ya Spika na katika eneo lile
wanakaa mawaziri. Ni eneo ambalo linalindwa wakati wote lakini watu
wasiojulikana wameweza kupita na kufanya uhalifu.
Anasema tayari baraza hilo lilikwishamwandikia barua Mkuu wa Jeshi la
Polisi nchini (IGP) Simon Sirro kuhusu tishio la usalama wa kiongozi
huyo lakini hakujibu.
“Agosti 24 nilimuandikia barua IGP kuhusu hofu ya usalama wa kiongozi
wetu kama ambavyo taratibu zinaruhusu kutoa taarifa hata kama hofu hiyo
haipo juu yako lakini jana amesema kuwa hakuwa na taarifa rasmi za
Lissu,” anasema na kuendelea
‘’Endapo Jeshi la Polisi linasita kuchukua hatua vijana hao
watachukua jukumu la kuwashughulikia watu hao wasiojulikana kwa namna
isiyojulikana ili mradi kulinda hali ya usalama wa nchi kama lilivyo
jukumu la kila Mtanzania’’ anasema
Anasema utaratibu huo ukishindikana atajiuzulu kwa sababu atakuwa ameshindwa kusimama kama kiongozi wa vijana.
“Natoa agizo kwa viongozi wote wa vijana nchi nzima kuratibu na
kuonyesha namna wanavyokerwa na vitendo hivi vya uvunjifu wa amani,
zoezi hili lifanyike kwa namna isiyojulikana na siku isiyojulikana,”
amesema.
Kwa upande wake Katibu wa baraza hilo Julias Mwita amesema Bavicha
wamewahi kutoa taarifa kuwa nchi inavimba kutokana na matendo ya
viongozi wa Serikali hasa wateule wa Rais lakini taarifa yao ilipuuzwa.
“Matendo ya viongozi hao yanachochea yanajenga chuki na uhasama
miongoni mwa watu. Hata Lissu alitoa taarifa kuhusu usalama wake
akapuuzwa lakini ungekuwa uchochezi angefuatiliwa,” anasema Mwita.
Anasema jeshi la polisi linapaswa kuwa sikivu na vijana wote
wakakamavu na wenye uwezo wa kuhoji katika taifa hili wasikubaliane na
mambo yanayokwenda kinyume na matakwa ya Watanzania
No comments:
Post a Comment