Waziri Mkuu aagiza halmashauri zote nchini kuwa na ofisi ya TRA - TANZA MEDIA ONLINE

Friday, 11 August 2017

Waziri Mkuu aagiza halmashauri zote nchini kuwa na ofisi ya TRA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameziagiza halmashuri zote nchini kuwa na ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuweza kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato katika maeneo yao.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo  wakati akizungumza na viongozi pamoja na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora.

Amesema TRA ndio chombo cha serikali kilichopewa Mamlaka ya kisheria katika  kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya serikali na kuwezesha utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.

Ameongeza kuwa uwepo wa Mamlaka hiyo katika kila halmashauri ni muhimu sana kwa kuwa uwatashirikiana kupeana mbinu za namna ya kufanikisha zoezi zima la ukusanyaji mapato kutoka katika vyanzo mbalimbali vilivyopo.

Aidha Majaliwa Amesema halmashauri zote zimepewa jukumu la kuhakikisha zinakusanya mapato yake kwa Zaidi ya  asilimia 80  ili kufanikisha utekelezaji wa mipango na kurahisisha utekelezaji wa  miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amewataka Wakurugenzi, madiwani na watendaji wa vijiji na kata kushirikiana kwa ukaribu zaidi ili kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato na kufanikisha malengo ya serikali.

Hata hivyo Majaliwa Ameipongeza halmashauri za Kaliua, Nzega Mji na Nzega DC kwa kufanikisha lengo hilo na kuziagiza halmashauri 5 za mkoa huo zilizoshindwa kufikisha lengo la serikali la kukusanya asilimia 80 ya bajeti yake kuongeza juhudi katika makusanyo yao.

No comments:

Post a Comment