Kufuatia madai mazito yaliyotolewa na Tundu Lissu, Mbunge wa Singida
Mashariki na mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), kwamba ndege ya serikali aina ya Bombadier iliyotakiwa kutua
nchini mwezi Juni, imezuiliwa na watu wanaoidai serikali, Ofisi ya
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, imetoa
taarifa ya kupinga vikali kauli ya Lissu na wenzake na kutoa ufafanuzi.
Katika taarifa iliyotolewa leo, Agosti 19, 2017 katika Ukumbi wa
Idara ya Habari, Maelezo, msemaji mkuu wa serikali amewahakikishia
Watanzania kuwa ndege hiyo ipo na itakuja nchini, na kwamba taratibu za
kidiplomasia na za kisheria zinaendelea ili kuhakikisha kuwa ndege hiyo
inakuja nchini na kuanza kutoa huduma.
Aidha, katika taarifa hiyo, msemajai mkuu wa serikali, amewataka
wananchi kuwa makini na wanasiasa wanaotafuta umaarufu, kwani zipo
taarifa zinazoonesha kwamba wanasheria walioizuia ndege hiyo,
walishawishiwa na wanasheria kutoka nchini, wasioitakia mema serikali
inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
“Wanasheria hao waliokwenda kufungua madai kwamba serikali yetu
inadaiwa na kwamba ndege hiyo ishikiliwe, hawana uhalali wowote wa
kufanya hivyo na ni matapeli tu ambao wamesukumwa na baadhi ya viongozi
wa kisiasa wasioitakia mema nchi yetu,” ilikaririwa sehemu ya taarifa
hiyo.
Aidha, taarifa hiyo iliendelea kueleza kwamba, wapo wanasiasa nchini
ambao wanakingia kifua mambo ambayo yanarudisha nyuma maendeleo ya nchi,
ikiwemo kuwashawishi wafadhili wasilete misaada tena Tanzania, kubeza
jitihada za kunusuru madini na maliasili za nchi na wanaobeza juhudi za
Rais Magufuli katika kuhakikisha kuwa maisha ya Watanzania, hasa wa hali
ya chini, yanaboreshwa.
No comments:
Post a Comment