Rais Dkt Magufuli akiwa na wananchi wa kada mbalimbali feri jijini Dar es salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 25 Agosti, 2017 amefanya ziara
ya kushtukiza katika eneo la Feri na kisha kuvuka bahari kwa kutumia
kivuko cha MV Kigamboni ambako amekutana na wananchi wa Kigamboni,
ametembelea Chuo cha Kumbukumbu ya Mwl. Nyerere na ametembelea Daraja la
Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Baada ya kukata tiketi yake Mhe. Rais
Magufuli amepata wasaa wa kuzungumza na wananchi aliosafiri nao katika
kivuko cha MV Kigamboni na baadaye kuzungumza na wananchi wa Kigamboni
ambapo ameulizwa na kujibu mambo mbalimbali.
Kuhusu ubovu wa barabara Mhe. Rais
Magufuli amesema Serikali imechukua hatua ya kukabiliana na tatizo hilo
kwa kuanzisha Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) ambayo itafanya kazi ya kutengeneza barabara kwa kiwango cha lami.
Kuhusu tatizo la kukatika kwa umeme
amesema Serikali inatekeleza miradi mbalimbali itayoongeza kiwango cha
umeme katika gridi ya taifa pamoja na kurekebisha miundombinu yake na
amewaomba kuwa na subira wakati juhudi hizo zinaendelea.
Akiwa katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwl. Nyerere Mhe. Rais Magufuli amekutana na vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kutoka vyuo na vyuo vikuu vya Mkoa wa Dar es Salaam waliopiga kambi
katika chuo hicho, ambao wamempongeza kwa kazi kubwa na nzuri
anayoifanya kuiongoza Serikali ya Awamu ya Tano ambayo kwa muda mfupi
imeonesha uongozi unaoacha alama.
Vijana hao wamemhakikishia kuwa
wanamuunga mkono na wamemuahidi kuwa wapo tayari kuitumikia nchi kwa
jukumu lolote watakalopewa na kwamba daima watatanguliza maslahi ya
nchi.
Akizungumza na vijana hao Mhe. Rais
Magufuli amewapongeza kwa moyo wa uzalendo waliouonesha, na amewataka
kuwa nguzo imara ya mabadiliko ya kweli nchini ili juhudi zinazofanywa
na Serikali ya Awamu ya Tano kurekebisha mambo yaliyosababisha kukiuka
misingi ya Waasisi wa Taifa zizae matunda.
Mhe. Rais Magufuli ameeleza baadhi ya
juhudi hizo kuwa ni kukabiliana na rushwa inayodhohofisha uchumi na
huduma za kijamii, kudhibiti mianya ya matumizi mabaya na upotevu wa
fedha na mali za umma, kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti vya
kughushi, kuongeza bajeti ya maendeleo katika bajeti ya Serikali,
kuongeza uzalishaji wa umeme, kujenga viwanda, kujenga reli, kununua
ndege za Serikali, kuongeza ukusanyaji wa kodi na kuchukua hatua kali
dhidi ya wahujumu uchumi.
“Nataka niwahakikishie
vijana wote kuwa nawapenda sana, hata mimi nilikuwa Umoja wa Vijana,
yote yaliyotokea kinyume na misingi ya chama hiki na misingi ya waasisi
wetu wakiongozwa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere nimeamua
kuyanyoosha na yatanyooka, na nyinyi simameni imara, kitumikieni chama
na msitumikie watu au vikundi vya watu, mkifanya hivyo kila kitu
kitakwenda vizuri kabisa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli amewataka vijana hao
kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa
chama utakaofanyika baadaye mwaka huu, na amebainisha kuwa wasiwe na
hofu ya kuwepo kwa rushwa kwa kuwa wote watakaojihusisha na vitendo vya
rushwa hawatapitishwa kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama.
Pia amewaambia viongozi wa Secretarieti
ya CCM aliowakuta wakizungumza na vijana hao kuwa anazo taarifa zote
juu ya watu waliojimilikisha mali za chama na amesema anasubiri wakati
ukifika achukue hatua zinazostahili.
Baada ya kuzungumza na vijana hao Mhe.
Rais Magufuli ametembelea Daraja la Nyerere na kuzungumza na wananchi wa
eneo hilo, ambapo amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul
Makonda kufanyia kazi ombi la wananchi kujengewa kituo cha Daladala.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
25 Agosti, 2017
No comments:
Post a Comment