Mtangazaji mkongwe wa
redio, Mike Mhagama, amesimulia jinsi alivyolianzisha jina ‘Bongo
Flava.’ Kupitia podcast yake mpya ‘Maktaba ya Bongo Flava’ itokayo kila
siku za Alhamis, amesema kipindi hicho alikuwa anaendesha kipindi cha DJ
Show cha Radio One akishirikiana na Sebastian Maganga.
Amesema kipindi hicho walikuwa wakicheza zaidi nyimbo za nje lakini
walikuja kuamua kutenga dakika 30 za kucheza aina fulani ya muziki
ukiwemo wa nyumbani.
“Ilipofika dakika 30 za muziki wa R&B siku hiyo nilikuwa kwenye
usukani na kwa mbwembwe nilicheza nyimbo ya kundi la R&B lililoitwa
Four Crews Flavour na baadaye kuiunganisha na wanadada wakali kabisa
wakati huo wakiitwa Unique Sisters,” anasimulia Mike.
“Kwa vile midundo, mpangilio, lugha na utaalam wa muziki wenyewe
kamwe huwezi kufananisha na ule wa Soul 4 Real kwa mfano au Sisters With
Voices kutoka Marekani, lakini tulipenda kutofautisha kati ya aina hizi
mbili za muziki na ndipo session hii niliibatiza jina ambayo
ingetofautisha R&B ya Marekani na ile ya kwetu. Niiipa session hii
jina la ‘Bongo Flava,’ hii ilikuwa mwaka 1996,” ameongeza.
“Na ndio ulikuwa mwanzo wa neno Bongo Flava, likiwa na maana ya
muziki wenye mahadhi ya nje lakini wenye vionjo na ladha ya Tanzania na
si vinginevyo. Lengo langu kuu kuupa muziki huu jina hili ni
kuutofautisha na muziki ule wa Marekani.”
Kwenye kipindi hiki pia Mhagama ameeleza jinsi mwaka 2007 alivyozima
ubishi wa baadhi ya watu waliokuwa wakijinadi kuwa ndio walianzisha neno
Bongo Flava. Anasema watu hao walialikwa na Clouds FM kwenda kuelezea
hoja yao mbele yake lakini waliingia mitini.
Kusikiliza kipindi hiki bofya link hii >> http://bit.ly/2uLMUK2 au download app ya Afripods kwenye App Store na Playstore
CHANZO:DIZZIMONLINE.COM
No comments:
Post a Comment