Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Nyakoro Sirro amefanya mabadiliko ya makamanda wa polisi mikoani.
Taarifa ambayo imetolewa na msemaji
wa Jeshi la Polisi Barnabas Mwakalukwa imesema kwamba Sirro amemteua
Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Juma Yusuf Ally kuwa Kaimu Kamishna wa
Polisi Zanzibar.
Uteuzi huo unafuatia kustaafu kwa
aliyekuwa Kamishna wa Polisi Zanzibar Kamishna Hamdani Omari Makame kwa
mujibu wa sheria baada ya kutimiza umri wa miaka sitini (60).
Kabla ya uteuzi huo DCP Juma alikuwa ni Mkuu wa Utawala na Fedha Makao Makuu ya Polisi Zanzibar. IGP
Sirro pia amemteua Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP)
Lazaro Mambosasa kuwa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam. Kabla ya uteuzi huo, SACP Mambosasa alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma.
Kufuatia uteuzi huo, aliyekuwa Kaimu
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam anakwenda kuwa Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mtwara, na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Neema Mwalimu Mwanga
anakwenda Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam.
IGP Sirro pia amemteua aliyekuwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke Kamishna Msaidizi Mwandamizi
wa Polisi (SACP) Gilles Bilabaye Mroto kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Dodoma na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Emmanuel Lukula kwenda kuwa
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Temeke.
Kabla ya uteuzi huo, ACP Lukula alikuwa Ofisa Mnadhimu wa Polisi mkoa wa Mbeya. Jeshi
la Polisi linatoa wito kwa wananchi wote kuendela kushirikiana na Jeshi
hilo kwa kufichua taarifa za uhalifu na wahalifu ili kwa pamoja
tuendelee kuiweka Tanzania salama.
No comments:
Post a Comment