ALIYEKUWA
kocha wa Simba SC, Muingereza Dylan Kerr amesema kwamba klabu hiyo
haitafanikiwa bila kuajiri Mkurugenzi wa Ufundi, mwenye vyeti vya
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) au la Ulaya (UEFA).
Katika
taarifa yake leo, Kerr aliyefukuzwa
wiki mbili zilizopita Simba SC, amesema kwamba Mkurugenzi wa Ufundi
anayetambuliwa na CAF au UEFA ni muhimu katika klabu kwa ajili ya
kufanya kazi kwa karibu na kocha.
Amesema
kwamba kwa sasa hali ilivyo ndani ya Simba shughuli nyingi za kiufundi
zinafanywa kienyeji na watu ambao hawana taaluma hiyo, ambao ndiyo
huajiri makocha, kusajili wachezaji na kufukuza pia.
“Klabu
haina hata Mjumbe mmoja wa bodi mwenye vyeti vya UEFA au CAF, ni hivi
karibuni tu Mjumbe mmoja amekamilisha mafunzo ya awali ya ukocha kwa
mara ya kwanza,”.
“Hadi
klabu itakapomteua Mjumbe mmoja wa bodi mwenye sifa, anayetambuliwa na
CAF au UEFA na mwenye uzoefu wa masuala ya soka, ili afanye kazi kwa
karibu na kocha katika masuala kama ya usajili wa wachezaji, mipango ya
mechi, mipango ya maandalizi ya kabla ya msimu, vifaa vya mazoezi,
msingi wa soka la vijana na masuala yahusuyo soka kwa ujumla, ndipo
itapiga hatua,”amesema.
Amesema
yeye si aina ya makocha waoga wa kupangiwa mambo na Wajumbe wa Bodi
ambao hawana sifa, vigezo wala uzoefu wa masuala ya soka, ambao siyo tu
wanataka kupanga timu (vikosi vya kucheza mechi), lakini pia kuwa na
mamlaka ya kusajili na kufukuza wachezaji.
Kerr
pia amesema amepitia matatizo mengi Simba SC ambayo hakuwahi kusema
katika kipindi chake cha kifupi cha kufanya kazi tangu Julai mwaka jana,
ikiwemo yeye na wachezaji kucheleweshewa mishahara hususan mwezi
Novemba na Desemba, lakini alivumilia.
Aidha,
Kerr amelalamikia maombi yake juu ya masuala ya kitaalamu na kiufundi
kutofanyiwa kazi na viongozi wa Simba SC, lakini baada ya kuondoka
yakafanyiwa kazi.
Amesema
aliomba mipira halisi ya Addidas itumike katika mechi zao na si ile ya
kiwango cha chini, ambayo wachezaji hawafurahii kuichezea, lakini
hakusikilizwa.
“Niliomba
pia nyasi za Uwanja wa Taifa zipunguzwe, zilikuwa ndefu sana na
kutuzuia kucheza vizuri kwa staili yetu. Sikutekelezewa. Ajabu sasa,
baada ya mimi kuondoka, mipira halisi ya Addidas ndiyo inatumika katika
mechi za Simba na nyasi za Uwanja wa Taifa zimepunguzwa,”amesema na
kuongeza; “Bravo (hongera) Simba, lakini kwa nini sasa tu, niliomba kwa
michezo 14 ya msimu, tuachane na hayo, hii ni kwa upande wangu, ninaweza
kuwa mwisho wa matatizo,”amesema.
Kuhusu
kufukuzwa kwake baada ya timu kutolewa katika Nusu Fainali ya Kombe la
Mapinduzi, Kerr amesema kwamba ni kinyume cha Mkataba wake wa miaka
miwili na klabu.
“Mkataba
wangu wa miaka miwili, ulikuwa wazi kwamba nitahukumiwa kutoakana na
matokeo ya Ligi Kuu mwishoni mwa msimu wa VPL wa 2015 - 2016 na matokeo
yangu yalikuwa bado yananiweka katika nafasi ya kupata tiketi ya kucheza
michuano ya Afrika mwaka 2017, tungefuzu,”amesema.
“Naweza
kuthibitisha hakuna kipengele kilichowekwa katika Mkataba wangu juu ya
matokeo ya mechi za mashindano mengine au ile michuano ya Zanziba (Kombe
la Mapinduzi) hivi karibuni,”.
“Niliamini
kuwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, huku tukiendelea
kupambana kupanda nafasi ya pili au ya kwanza, nilikuwa kwenye nafasi ya
kutimiza matakwa niliyopewa na uongozi,”amesema.
Amesema
amesikitishwa timu kutolewa katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi,
lakini alitaka kuyatumia mashindano hayo kwa ajili ya kuwaandaa
wachezaji kurejea kwenye ligi kwa ari na nguvu mpya ili waendelee
kuwania ubingwa.
Pamoja
na yote, Kerr ameushukuru uongozi wa Simba SC, wachezaji na wapenzi kwa
kipindi alichokuwa nao na kuwatakia heri chini ya zama mpya baada yeye
kuondoka.
Kwa sasa Simba SC ipo chini ya kocha Mganda, Jackson Mayanja ambaye mpango wa awali ilikuwa awe Msaidizi wa Kerr.
Kocha Kerr (kushoto) amesema kwamba Simba SC inahitaji Mkkrugenzi wa Ufundi, ili mambo yaende sawa |
Kerr katikati akipongezwa na viongozi na wanachama wa Simba SC baada ya kufunga bao katika mechi ya viongozi wa klabu hiyo dhidi ya Wasanii kwenye tamasha la Simba Day Agosti mwaka jana |
No comments:
Post a Comment