Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG, Prof. Mussa
Assad ametoa taarifa yake ya ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha za
umma kwa mwaka 2016/17. Kwa sasa taarifa hiyo iko wazi kwa umma, baada
ya kuwa imekabidhiwa rasmi bungeni. Sisi ACT Wazalendo, tumeisoma,
kuipitia na kuichambua taarifa husika, kwa lengo la kuitumia ili
itusaidie kutimiza wajibu wetu wa kuisimamia Serikali, kama chama cha
Upinzani bungeni.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndugu Magufuli tayari amechukua hatua za kiuwajibikaji dhidi ya baadhi ya Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa zenye hati isiyoridhisha, hatua hii ni ya njema, ACT Wazalendo tunampongeza kwa jambo hilo. Hata hivyo, baada ya kuipitia ripoti husika, tumegundua kuwa CAG ameibua masuala mazito ambayo yana madhara makubwa kwenye mfumo mzima wa Bajeti ya Nchi kama hayatashughulikiwa. Tumewaita hapa kuyazungumzia hayo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndugu Magufuli tayari amechukua hatua za kiuwajibikaji dhidi ya baadhi ya Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa zenye hati isiyoridhisha, hatua hii ni ya njema, ACT Wazalendo tunampongeza kwa jambo hilo. Hata hivyo, baada ya kuipitia ripoti husika, tumegundua kuwa CAG ameibua masuala mazito ambayo yana madhara makubwa kwenye mfumo mzima wa Bajeti ya Nchi kama hayatashughulikiwa. Tumewaita hapa kuyazungumzia hayo.
Maeneo 8 ya Hatari Katika Ripoti ya CAG.
1. Mawaziri Wanavunja Sheria ya Ukaguzi. Tunaomba kutoa angalizo na
muongozo wa kisheria juu ya hadaa inayofanywa na Serikali juu ya
kinachoitwa “Majibu ya Mawaziri juu ya Ripoti ya CAG”. Kisheria Mikutano
hii ya Mawaziri na wanahabari inayoendelea ni kinyume na Sheria ya
Ukaguzi ya Umma, kifungu cha 38(1) na (2), ambacho kinaelekeza waziwazi
kuwa Maafisa Masuuli ndio wanapaswa kujibu hoja za ukaguzi zilizoibuliwa
na CAG, tena majibu husika hupaswa kuletwa mbele ya Kamati za Bunge za
PAC na LAAC. Kwa utaratibu wa kawaida wa kiwizara, maafisa masuuli ni
Makatibu Wakuu wa Wizara na si Mawaziri.
2. 6% ya Fedha zilizokusanywa na Serikali hazijulikani zilizokwenda.
Katika ukaguzi wa Bajeti ya mwaka 2016/17, ambayo ni Bajeti ya kwanza ya
Serikali ya awamu ya tano, CAG ameonyesha kuwa kati ya Bajeti ya
shilingi 29.5 trilioni iliyoidhinishwa na Bunge, Serikali iliweza
kukusanya shilingi 25.3 trilioni tu kutoka vyanzo vyote vya kodi, vyanzo
visivyo vya kodi, mikopo ya ndani na nje, na misaada ya wahisani na
washirika wa maendeleo. Serikali ilishindwa kukusanya kiasi cha shilingi
4.2 trilioni, sawa na 15% ya Bajeti yote ya mwaka 2016/17. Jambo la
kushtusha na linalohitaji majibu ya Serikali ni kwamba, CAG amegundua
kuwa katika fedha zote zilizokusanywa, shilingi 25.3 trilioni, ni
shilingi 23.8 trilioni tu ndio zilitolewa kwa ajili ya mishahara ya
watumishi, matumizi mengine, matumizi ya maendeleo na kulipa madeni
yatokanayo na amana za serikali na riba, shilingi 1.5 trilioni
zilizobaki hazijulikani zimekwenda wapi. Fedha hii ambayo matumizi yake
hayajulikani ni sawa na 6% ya Fedha zote zilizokusanywa mwaka huo.
Matrilioni haya ambayo Serikali imeyapoteza ni zaidi ya mara mbili ya
Bajeti ya Wizara ya Maji ya mwaka husika (672 bilioni).
3. Bajeti ya Tanzania haina Hadhi (Credibility) tena. Taarifa ya CAG
inaonyesha kuwa Bajeti inayopitishwa na Bunge haina Hadhi (Credibility)
tena, kwani kuna matumizi makubwa ya nje ya Bajeti kinyume na
ilivyoidhinishwa na Bunge. Kwa mfano, CAG ameonyesha kuwa Bunge lilitoa
Kibali kwa Serikali kukopa mikopo ya ndani yenye thamani ya TZS 5.4
trilioni lakini Serikali ilikopa zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa kwa
10%, ambapo zilikopwa shilingi 5.9 trilioni, yaani bilioni 500 zaidi ya
ukomo wa kukopa uliotolewa na Bunge. Haya ni matusi makubwa kwa Bunge,
yanaondoa hadhi ya bajeti inayopotishwa na Bunge.
4. Heshima na Hadhi ya Bunge letu vinaondolewa. Kazi Kuu ya Bunge ni
kuidhinisha Bajeti inayoletwa bungeni na Serikali, mara baada ya
mjadala. Kwa sasa heshima na hadhi ya Bunge vinaondolewa kutokana na
Bajeti iliyopitishwa kutokutekelezwa, hasa kwa kiasi cha fedha
zilizoidhinishwa na bunge kwaajili ya miradi ya Maendeleo kutokutolewa.
Taarifa ya CAG imeonyesha kuwa, kwa ujumla, ni 68% tu ya Bajeti ya
Maendeleo ndio ilitekelezwa, hali ni mbaya zaidi kwa upande wa Serikali
za Mitaa, ambapo ni 51% tu ndiyo ilitekelezwa.
5. Mabilioni ya Fedha za Watanzania yametumika kulipa Madeni ambayo
hayakuidhinishwa na Bunge. Taarifa ya CAG imeonyesha pia kuwa Serikali
ilitumia zaidi ya shilingi 219 bilioni, kulipa madeni ya nyuma. Lakini
matumizi hayo hayakuwa sehemu ya Bajeti iliyoletwa na Serikali na
kuidhinishwa na Bunge. Hivyo madeni hayo ni hewa, na ulipwaji wake ni
matumizi nje ya Bajeti iliyopitishwa na Bunge.
6. TRA Wametoa Takwimu za Uongo za Mapato ya Kodi ya zaidi ya
shilingi 2.2 trilioni. Taarifa ya CAG imeonyesha, kwa mwaka wa fedha wa
2016/17, Mamlaka ya Mapato nchini, TRA ilituhadaa kwa kutangaza kuwa
imekusanya fedha zaidi kuliko uhalisia wake. Kati ya kiasi cha shilingi
15.1 trilioni ambazo TRA ilitutangazia kuwa imezikusanya kwa mwaka
2016/17, shilingi 2.2 trilioni hazikuwa za TRA. Kimsingi fedha hizo si
makusanyo ya kodi, bali TRA walizikusanya tu kama wakala wa asasi,
taasisi na wakala nyengine za Serikali. Makusanyo halisi ya fedha za
kodi yalikuwa ni shilingi 12.9 trilioni tu. Uongo huu wa TRA kutangaza
hata mapato yasiyo yake umepelekea kutokea kwa shilingi 325 bilioni
ambazo zilihesabiwa mara mbili (double accounting) kwenye Hesabu Jumuifu
za Taifa, na hivyo kuchafua hesabu za Taifa na kuondoa uhalali wake
kitakwimu. Pia taarifa ya CAG imeonyesha kuwa TRA hudanganya makusanyo
wanayotangaza kila miezi mitatu.
7. Serikali kwa ujumla imepata Hati Chafu. Taarifa ya CAG ya Ukaguzi
wa kwanza wa makusanyo na matumizi ya kibajeti ya Serikali ya awamu ya
tano, imeonyesha kuwa, kwa ujumla, Serikali ya Jamhuri ya Muungano
imepata Hati Chafu, kwa kuwa Hesabu Jumuifu za Taifa (consolidated
accounts) zimepata Hati ISIYORIDHISHA (Chafu). Sababu za kutolewa Hati
hii kwenye taarifa ya CAG ni pamoja na fedha kutumika kinyume na mafungu
yaliyopangwa na Serikali yenyewe, kupotea kwa shilingi 1.5 trilioni,
TRA kutangaza mapato ambayo si yake kuwa ni yake na hivyo kupelekea
‘double accounting‘ (kuhesabiwa mara mbili kwa fedha) kwenye mapato.
Hesabu Jumuifu za Taifa ndio Hazina ya Taifa, kupata Hati Chafu ni
hatari sana kwa mustakabali wa Taifa.
8. CAG hajakagua Ununuzi wa Ndege. Licha ya kuwa taarifa hii ya CAG
ni taarifa bora sana kwa maudhui na uchambuzi, kuna mambo kadhaa ambayo
CAG ameyaacha, ikiwemo Ununuzi wa Ndege za Shirika la Ndege Nchini, ATCL
ambao kwa sehemu umefanyika mwaka wa fedha 2016/17.
Mapendekezo: Baada ya kusoma taarifa hiyo ya CAG na kuyaanisha maeneo hayo 8, sisi ACT Wazalendo tuna mapendekezo yafuatayo:
1. Tunawaomba Wenyeviti wa Kamati za Bunge za PAC na LAAC kufikisha
suala Mawaziri kuzungumza kwenye vyombo vya habari kujibu ripoti ya CAG
kwa Spika wa Bunge, ili Spika amjulishe Waziri Mkuu juu uvunjifu huu wa
sheria unaofanywa na Mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano, wakiwemo
Mawaziri wazoefu wa taratibu za kibunge kama Waziri William Lukuvi na
Waziri Harrison Mwakyembe. Mawaziri hawa wanafanya ‘spinning’ (hadaa)
ili kuficha madudu ambayo CAG ameyaibua. Tunawaasa waache jambo hili, na
wafuate sheria.
2. Tunaisihi Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, PAC kuomba kibali
cha kukutana haraka na kuagiza Ukaguzi Maalumu wa shilingi 1.5 trilioni
ambazo zimepotea na Serikali ya Awamu ya Tano imeshindwa kuzitolea
maelezo kutoka kwenye makusanyo ya mwaka 2016/17. Hii ni mara ya kwanza
kwenye historia ya nchi yetu kwa Serikali kukusanya fedha, kutozigawa
kwenye Wizara, Idara, Wakala na Mikoa, kutoonekana matumizi yake na CAG
kushindwa kuzikagua. PAC itimize wajibu wake haraka iwezekavyo. Wakati
huu ukaguzi huu unafanyika, kama ilivyofanyika kwa Wakurugenzi wa
Mamlaka za Serikali za Mitaa waliopata Hati Isiyoridhisha, Rais
amsimamishe kazi Katibu Mkuu Hazina na Mlipaji Mkuu wa Serikali, kwa
kushindwa kusimamia vema Fedha za Umma na kupelekea Hesabu Jumuifu za
Taifa (consolidated accounts ) kupata Hati isiyoridhisha ili kupisha
uchunguzi huu.
3. Tunalishauri Bunge litake maelezo ya kina ya Serikali kuhusu
kukopa bilioni 500 zaidi ya Serikali yenyewe ilivyoomba na kuidhinishiwa
na Bunge. Ni matarajio yetu kuwa Bunge litachukua hatua dhidi ya
Serikali kwa kukiuka Sheria ya Bajeti ambayo inakataza kabisa Serikali
kukopa zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa na Bunge. CAG ameonya katika
Taarifa yake kwa kusema yafuatayo kuhusu jambo hili “sehemu kubwa ya
mtaji wa mabenki unakuwa umefungwa kwenye fedha walizokopesha serikali
kwa muda mfupi na muda mrefu; na matokeo yake, riba ya kukopesha kwa
watu binafsi inakuwa kubwa na gharama za maisha zinakuwa juu”. Ukopaji
wa namna hii unafanya UCHUMI KUSINYAA kwani unaondoa fedha kwenye
mzunguko na kushusha uzalishaji.
4. Tunalishauri Bunge liiwajibishe Serikali kwa kutoheshimu Bajeti
ambayo Bunge lilipitisha. Bunge linapaswa kulinda hadhi na heshima yake
kwa kuhakikisha fedha za maendeleo linazozipitisha zinapelekwa kama
ilivyopangwa. Bunge lisipofanya hivyo litaendelea kudharaulika. Spika wa
Bunge asimame imara kulinda Mhimili wa Bunge dhidi ya uvunjifu wa
sheria wa Serikali kwenye masuala ya Fedha za Umma, hasa wakati huu
ambao CAG ameonyesha Fedha nyingi zimetumika kinyume na utaratibu huku
fedha za maendeleo zilipitishwa na Bunge zikiwa hazipelekwi.
5. Ni imani yetu kuwa Bunge litawawajibisha wote waliohusika katika
malipo ya madeni ambayo hayakuidhinishwa na Bunge letu. Madeni haya pia
yanapaswa kujulikana ni yepi kwani CAG anaonyesha kuwa Wizara ya Ujenzi
ndiyo imelipa zaidi madeni ya namna hii ambayo hayakuwa kwenye bajeti.
Utaratibu wa namna hii ukiachwa bila kuchukua hatua, utatoa mwanya wa
fedha za umma kupotea tu bila maelezo yoyote.
6.TRA kwa makusudi, na kwa lengo la kufanya hadaa walitangaza kiwango
kikubwa zaidi cha makusanyo kuliko kiwango ilichopaswa kutangaza kuwa
imekusanya. Tunatarajia kuwa Bunge litaitaka TRA iombe radhi Watanzania
kwa upotoshaji huo ilioufanya na kutaka wote waliohusika kwenye hadaa
hii wawajibike. Pia tunawasihi TRA kuzingatia weledi wa kazi yao kwa
kutangaza makusanyo yao tu, na kuacha fedha za taasisi na asasi nyengine
kama VETA, TPA, Bodi ya Mikopo nk (ambazo TRA huzikusanya kama Wakala
wa taasisi hizo) zitangazwe na wahusika wenyewe.
7. Tunaishari Serikali kurejesha utaratibu wa kupanga matumizi ya
kila mwezi ya fedha za umma kwa Hazina, na kuacha utaratibu wa sasa wa
Ikulu kupanga matumizi ya kila mwezi. Utaratibu huu wa sasa unamuexpose
(unamweka kwenye mazingira hatari) Rais, hasa kutuhumiwa kwa ufisadi na
kukiuka sheria iwapo kuna makosa ya upotevu wa fedha kama haya ambayo
CAG ameyaibua katika taarifa yake na kupelekea hesabu jumuishi za
Serikali kupewa Hati Chafu. Tunashauri pia kuachwa kwa mfumo wa Rais
wetu kutamka kugawa Fedha kinyume kabisa na Bajeti iliyopitishwa na
Bunge.
8. Ni matatajio yetu kuwa katika ripoti ya mwakani ya CAG, Taifa
litapata wasaa wa kuona ukaguzi wa ununuzi wa ndege za shirika la ndege
la Taifa, ATCL na ukaguzi wa manunuzi ya kandarasi ya ujenzi wa kiwanja
cha ndege cha Chato. Ni muhimu sana kwa CAG kuona mambo yanayosemwa na
umma na kuchukua hatua za ukaguzi kwani yeye ndiye mlinzi wa fedha za
umma.
Hitimisho
ACT Wazalendo tunawasihi Wabunge wote bila kujali vyama vyao
kutekeleza wajibu wao wa kuisimamia Serikali. Wabunge tusipotekeleza
wajibu wake nchi yetu itaangushwa na matumizi mabovu ya nje ya Bajeti na
ya kinyume cha sheria. Ni dhahiri, kwa dalili hizi zilizoonyeshwa na
taarifa ya CAG, kuwa Wabunge tusipoisimamia na kuidhibiti Serikali ya
awamu ya tano, Nchi itafilisika kutokana na maamuzi ya hovyo, yasiyo ya
kibajeti, yanayoenda kinyume na kanuni za kifedha na kiuchumi, na
yasiyozingatia sheria za Nchi yetu.
Sisi ACT Wazalendo tutaendelea kuichambua taarifa hii ili kuibua
masuala zaidi. Haya tuliyoyaeleza leo ni machache sana, hatujagusia
kabisa mapungufu kwenye deni la Taifa, kulinganisha na mambo mengi
ambayo CAG ameeleza. Tunawahimiza Wabunge na Wananchi kwa ujumla kusoma
taarifa ya CAG kwa ukamilifu. Taarifa ya mwaka huu ina hoja nzito kuliko
wakati mwingine wowote ule. Haijawahi kupata kutokea Serikali ya Nchi
kulidgarau Bunge letu kama ilivyo kwa kiwango kilichoonyeshwa na taarifa
ya mwaka huu ya CAG.
Ahsanteni Sana.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge, Kigoma Mjini
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Bungeni Dodoma
Aprili 15, 2018
No comments:
Post a Comment