YANGA imewapa
maneno matamu mashabiki wake kwa kusema sasa kikosi chake kimekaa sawa
na kipo kamili kuweza kushinda mechi ya leo Jumamosi dhidi ya Lipuli FC.
Yanga inacheza mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara kuanza mzunguko wa pili
ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa huku ikiwa imetoka
kushinda mechi ya 32 Bora ya Kombe la FA dhidi ya Ihefu FC.
Katika mchezo dhidi ya Ihefu, Yanga ilibanwa hadi dakika ya 90
iliposawazisha na kumaliza kwa sare ya bao 1-1 kisha ikashinda kwa
penalti 4-3, kiwango cha Yanga siku hiyo hakikuwafurahisha baadhi ya
mashabiki wake.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa amewaambia mashabiki wa
timu hiyo kuwa, kikosi chao kipo sawa hivi sasa na kikubwa wanataka
pointi tatu kwa wapinzani wao Lipuli.
Yanga ina pointi 28 katika nafasi ya tatu, imesema inataka kushinda
mechi hiyo ili kupunguza tofauti ya pointi dhidi ya Simba na Azam FC
zilizo juu yake. Simba ipo kileleni na pointi 35, Azam ya pili ina
pointi 30.
Nsajigwa ambaye ni nahodha na beki wa zamani wa Yanga, aliliambia Championi Jumamosi kuwa, maandalizi yote ya mchezo huo yamekamilika na wataingia uwanjani kwa ajili ya kushinda tu.
“Hakuna mechi nyepesi kwetu, kila mechi tunaichukulia kama fainali na
kikubwa tunataka kupunguza idadi ya pointi ambazo wapinzani wetu Simba
wanaongoza katika ligi.
“Tunashukuru timu imekaa sawa sasa, tupo vizuri na hakuna majeruhi
aliyepatikana baada ya mechi na Ihefu, timu itaingia uwanjani kwa lengo
moja la ushindi, pia nafurahi morali ya wachezaji ipo juu sana.
“Hatutawadharau wenyeji kwani tulitoka nao sare katika mzunguko wa
kwanza, hivyo watapambana kushinda nyumbani ila sisi pia tutapambana
kushinda,” alisema Nsajigwa anayemsaidia bosi wake George Lwandamina.
Wakati huohuo, Kocha wa Lipuli, Selemani Matola akizungumzia mchezo
huo, alisema: “Sisi tumejiandaa vizuri na tumemaliza kazi ya kuwapa
mbinu mbalimbali za ushindi wachezaji wetu ili tushinde.
“Tutacheza kwa tahadhari kwani wapinzani wetu wana wachezaji wengi
wenye uzoefu wa kimataifa kama Tshishimbi (Papy), Chirwa (Obrey) na
Yondani (Kelvin), hawa wanaweza kutupa ugumu.”
Matola ambaye timu yake ipo nafasi ya saba na pointi 16, alisema
anafurahia kupona kwa beki wake Joseph Owino aliyekuwa akisumbuliwa na
nyama za paja.
chanzo:globapublisher online

No comments:
Post a Comment