Mohamed Salah amempiku mchezaji mwenzake wa Liverpool, Sadio Mane na
mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang kutwaa Tuzo
ya Mchezaji wa Afrika wa Mwaka 2017.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri aliibuka mshindi katika
kinyang’anyiro hicho dhidi ya wachezaji wenzake katika mkutano wa Tuzo
za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika mjini Accra.
Salah, ambaye ataikosa mechi ya Kombe la FA raundi ya tatu dhidi ya
Everton, Ijumaa usiku, amefurahia mwaka wa mafanikio kwa klabu na kwa
taifa lake pia.
Baada ya kufunga mara 10 akiwa Roma kati ya Januari na Mei, mchezaji
huyo mwenye umri wa miaka 25 aijiunga na Liverpool kwa uhamisho wa
rekodi kwa klabu hiyo na kwa haraka ameshafanikiwa kuweka kimiani magoli
24 katika michuano yote.
Akiongea kuelekea hafla hiyo, Salah aliwaambia waandishi: “Nadhani
tuna timu bora ya taifa na tumefanya vizuri kwenye Kombe la Afrika na
kufuzu Kombe la Dunia.”
Salah pia alizifumania nyavu mara mbili katika ushindi wa Misri wa
2-1 dhidi ya Congo kufuzu Kombe la Dunia Oktoba kuhakikisha timu yake ya
taifa inapata tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza
baada ya miaka 28.
No comments:
Post a Comment