Polisi nchini Kenya
wamemkamata mbunge mmoja ambaye 'alihusika' pakubwa katika hafla ya
kumuapisha kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga kuwa 'rais wa
wananchi'.
Kukamatwa kwa mbunge huyo wa upinzani kunajiri wakati ambapo serikali imefunga vituo vitatu vya runinga mbali na vile vya redio.
Tom Kajwang alikamatwa na kundi la maafisa wa polisi waliokuwa wamevalia nguo za raia, mjini Nairobi.
Kukamatwa
kwa kiongozi huyo kunajiri muda mfupi baada ya onyo kutoka kwa waziri
wa usalama kwamba watu waliohusika katika kumuapisha Raila Odinga
watakamatwa na kushtakiwa.
Vituo kadhaa vya runinga nchini Kenya vimefungiwa baada ya
mamlaka ya mawasiliano kuzima mitambo yao kwa kujaribu kupeperusha moja
kwa mkutano huo wa upinzani
Sherehe ya kuapishwa kwa Raila
ilichukuliwa na wengi kama mzaha lakini serikali imeshikilia kuwa ni
kitendo cha uhaini na kuhakikisha taarifa hiyo haitawafikia Wakenya
wengi waliokuwa wakiifuatilia tukio hilo.
Waziri wa usalama nchini
Kenya Dr Fred Matiangi amesema kuwa runinga hizo zitaendelea kufungwa
hadi uchunguzi kuhusu kuhusika kwao na kundi la pingamizi dhidi ya
serikali NRM linalohusishwa na muungano wa Nasa alilolipiga marufuku
utakapokamilika.
Vifaa vya kurusha matangazo vya vituo vya runinga
vya Nation Media Group NTV, Citizen TV cha kampuni ya Royal Media
services Limited na KTN vilizuiwa kurusha matangazo katika kituo cha
kurusha matangazo cha Limuru huku kituo cha kitaifa cha KBC na K24
kinachohusishwa na Rais Uhuru Kenyatta vikiendelea na matangazo yao.
Tangazo hilo la Matiangi linajiri huku kukiwa na malalamishi miongoni mwa raia kufuatia hatua hiyo ya serikali.
Katibu
mkuu wa shirika la wafanyikazi nchini Kenya COTU Francis Atwoli
ameishutumu serikali kwa kuingilia uhuru wa vyombo vya habari.
Bwana
Atwoli ambaye alizungumza mjini Nairobi amesema kuwa hatua hiyo ni
kinyume na sheria na inaenda kinyume na katiba ya Kenya ambayo inatoa
Uhuru wa vyombo vya habari na kupata habari.
''Serikali inafaa
kuharakisha na kurejesha matangazo ya runinga hizo. Sio makosa tu bali
pia ni kinyume cha katiba kuendelea na biashara yao ya kuwahabarisha
Wakenya'', alisema Atwoli.
Kufungwa kwa vituo hivyo kunajiri baada
ya mwenyekiti wa shirika la wahariri Kenya Linus Kaikai kudai kwamba
rais Uhuru Kenyatta alikuwa ametishia kuvifunga vyombo vya habari
vitakavyojaribu kupeperusha matangazo ya kuapishwa kwa viongozi wa NASA.
Kulingana
na Kaikai , vitisho hivyo vilitolewa katika ikulu ya rais tarehe 26
Januari baada ya wamiliki wa vyombo vya habari kuitwa na kutakiwa
kutorusha matangazo hayo.
No comments:
Post a Comment