Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa
maagizo kuhusu matumizi ya fedha za kigeni katika Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na kusisitiza kuwa utekelezaji wake uanze tarehe 1 Januari,
2018.
Maagizo hayo ni kama ifuatavyo: –
i. Bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania. Bei hizi
zinajumuisha kodi ya nyumba za kuishi na maofisi, bei ya ardhi, gharama
za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki.
ii. Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi
zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza
kufanyika kwa fedha za kigeni. Bei hizi zinajumuisha gharama za
usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania, gharama za mizigo
bandarini kwenda nchi za nje, gharama za viwanja vya ndege na viza kwa
wageni, na gharama za hoteli kwa watalii kutoka nje ya nchi. Walipaji
wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi
za kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni.
iii. Viwango vya kubadilishana fedha vitakavyotumika katika kuweka
hizo bei katika sarafu mbili viwekwe wazi na visizidi vile vya soko.
Ifahamike wazi kuwa ni mabenki na maduka ya fedha za kigeni tu
yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na
ushindani katika soko la fedha za kigeni.
iv. Mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yeyote hapa nchini kwa fedha za kigeni.
Aidha Dkt. Mpango ameviagiza vyombo vya dola viwachukulie hatua za
kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo haya ya Serikali.


No comments:
Post a Comment