WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willium Lukuvi
ameshiriki zoezi la uvunjaji wa nyumba kwa kuvunja nyumba yake kwa
hiari iliyokuwa imejengwa ndani ya hifadhi ya barabara ili kupisha
upanuzi wa barabara.
Waziri Lukuvi amevunja nyumba yake
iliyokuwa imejengwa katika eneo la hifadhi ya barabara kuu iendayo
katika hifadhi ya Ruaha katika Kijiji cha Mapogolo, mkoani Iringa.
“Kama kiongozi nimeamua kuonyesha
mfano kumuunga mkono Mhe. Magufuli ambaye ameamua kuiboresha barabara
hii kuwa kiwango cha lami mpaka Ruaha National Park ili kuongeza mapato
ya nchi lakini pia kuongeza vipato kwa wananchi wa barabara hii
wanayoitumia”.
“Kwa faida hizo nimeamua mimi
mwenyewe kuvunja leo hii nyumba ili wananchi wa eneo hili ambao barabara
hii itajengwa lazima wahakikishe wanabomoa wenyewe nyumba zao,” alisema
Waziri Lukuvi.
Aidha Waziri Lukuvi aliwataka
wananchi wote waliojenga ndani ya eneo la hifadhi ya barabara kuzivunja
wenyewe nyumba zao ili kurahisisha zoezi la upanuzi wa barabara hiyo uwe
wa muda mfupi, kwani barabara hiyo inajengwa kwa manufaa yao.
“Lazima tutii sheria bila shuruti.
Tuliowekewa alama ya X tuvunje nyumba zetu ili kazi ya ujenzi wa
barabara hii iwe nyepesi, gharama iwe ndogo na iende kwa muda mfupi,”
alisema Waziri.
Vilevile aliwakumbusha wakazi wa eneo
hilo ambao wamejenga ndani ya eneo la hifadhi ya barabara kuwa
wasitegemee fidia yoyote kutoka serikalini na badala yakee waanze
kuzibomoa nyumba zao pasipo kusubiri kuja kubomolewa kwa nguvu.
“Serikali haitolipa fidia kabisa kwa watu waliojenga kwenye eneo la barabara kama mimi,” alisema.
No comments:
Post a Comment