Matukio ya kuvamiwa watu na kupigwa
risasi yamekuwa yakiripotiwa siku za hivi karibuni ambapo September 7,
2017 liliripotiwa tukio la kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu kabla ya September 11, 2017 kuripotiwa
kushambuliwa Meja Jenerali Mstaafu Vicent Mritaba wakati anaingia getini
nyumbani kwake.
Matukio haya yamekuwa yakikemewa na watu mbalimbali na viongozi wa
kisiasa, dini, Taasisi na Serikali na kufuatia tukio la September 11 la
kupigwa risasa kwa Meja Jenerali Mstaafu Vicent Mritaba Chama cha ACT
Wazalendo kupitia kwa Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi, Ado
Shaibu jana September 12, 2017 kilitoa tamko kulaani.
Chama cha ACT Wazalendo kimepokea kwa masikitiko makubwa
taarifa ya kushambuliwa kwa risasi na kujeruhiwa kwa Meja Jenerali
mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) Vicent Mritaba kulikofanywa na
‘’Watu Wasiojulikana’’.
Kabla ya kustaafu, Meja Jenerali Vicent Mritaba amewahi
kuwa Mkuu wa Utumishi wa JWTZ. Akiwa kwenye nafasi hiyo, atakumbukwa kwa
msisitizo wake kwa wanajeshi kujiepusha na vitendo viovu hasa kuwapiga
raia na kujichukulia sheria mkononi ambavyo vinakwenda kinyume na wajibu
wa JWTZ wa kulinda mipaka ya nchi, raia na mali zao na kushiriki kazi
za kijamii.
Pia, Chama chetu kinalaani vikali uvamizi wa ofisi ya
Mawakili ya Prime Attorneys uliofanyika usiku wa kuamkia leo Jumanne 12
Septemba, 2017 jijini Dar es salaam.
Kuwepo kwa taarifa kwamba, pamoja na mambo mengine,
wahalifu hao waliiba kasiki lenye nyaraka mbalimbali za ofisi ni dalili
ya wazi kwamba hawakuwa wahalifu wa kawaida.
Vitendo hivi vya kuvamia na kuharibu ofisi za mawakili
ambavyo vimetamalaki hivi sasa, bila shaka vinatishia uhuru wa mawakili
katika utekelezaji wajibu wao kama Maafisa wa Mahakama.
Chama cha ACT kinalaani matukio yote haya mawili na
kuvitaka vyombo vya dola hasa Idara ya Usalama wa Taifa na Jeshi la
Polisi kuyachunguza matukio haya kwa umakini na kuhakikisha watekelezaji
wake wanafikishwa kwenye mkono wa sheria.
Ado Shaibu,
Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi
ACT Wazalendo.
Imetolewa leo tarehe 12 Septemba, 2017.
No comments:
Post a Comment