Imeelezwa kuwa jumla ya watoto wa kiume wapatao 40 wanaosoma kati ya darasa la
kwanza na la tatu kutoka visiwani Zanzibar wamefanyiwa ukatili wa
kuingiliwa kinyume na maumbile.
Hayo yameelezwa na Meneja wa mradi wa elimu ya
afya ya uzazi, haki za watoto na vijana, Dk. Ellen Otaru wakati
akizungumza na waandishi wa habari katika kongamano la madhimisho ya
Vijana Duniani lililofanyika kitaifa mjini Dodoma.
Dk. Otaru amesema kutokana na vitendo vya ukatikili wanavyofanyiwa
watoto hao wa kiume kunaweza kuwasababishia madhara makubwa ya kiafya
endapo watakosa msaada wa kimatibabu kwa kuwarejesha katika hali yao ya
kawaida.
Amesema sababu kubwa ya watoto kufanyiwa vitendo vya kinyama kwa
kuingiliwa kinyume na maumbile ni kutokana na kutotolewa kwa elimu ya
afya ya uzazi mashuleni.
Dk. Otaru mesema elimu ya afya ya uzazi inatakiwa ianze kutolewa
mashuleni kuanzia shule ya awali tofauti na sasa elimu hiyo inaanza
kutolewa kuanzia miaka 10 badala ya sita.
Amesema kama elimu ingetolewa mapema ni wazi kuwa watoto wa kiume
wangejua mapema kujikinga na watu wenye nia mbaya ya kutaka kuwalawiti
huku watoto wa kike wakiwa na maarifa ya kujiepusha na upatikanaji wa
ndoa na mimba za utotoni.
Hata hivyo ameitaja mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa tatizo la mimba
za utotoni kwa asilimia 53 ukifuatiwa na mkoa wa Tabora na huku akieleza
kuwa vitendo hivyo havitokani na umasikini tu bali hata ukosefu wa
elimu kwa jamii.
Pia alitoa wito kwa wazazi/walezi kuzungumza na watoto ili kuweza
kupata elimu ya afya ya uzazi ambayo itawasaidia na kujua madhara
atakayoyapata akitenda jambo hilo badala ya kuwaogopa watoto.
No comments:
Post a Comment