Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi
Benjamin Mchwampaka, ameanza ziara ya kazi ya takriban juma moja katika
mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa lengo la kukagua utekelezaji wa shughuli
mbalimbali za sekta hiyo.
Katika siku ya kwanza ya ziara hiyo,
Agosti 28 mwaka huu, Kamishna Mchwampaka alikutana na kuzungumza na
wafanyakazi wa Ofisi ya Madini, Kanda ya Ziwa Viktoria-Magharibi pamoja
na wafanyakazi wa Ofisi Ndogo ya Ukaguzi wa Madini Kanda ya Mwanza,
iliyokuwa ikijulikana kama Wakala wa Ukaguzi Madini Tanzania (TMAA).
Akizungumza mara baada ya kupokea
taarifa ya utendaji kazi wa Ofisi hizo mbili, Kamishna Mchwampaka
aliwataka wafanyakazi hao kufanya kazi kwa bidii na kwa ushirikiano ili
kufanikisha malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwaletea wananchi
wake maendeleo ya dhati.
Katika hatua nyingine, akizuru Mradi wa
Uchimbaji wa Kati wa Madini ya Dhahabu uliopo Ishokelahela wilayani
Misungwi, Mkoa wa Mwanza, Kamishna Mchwampaka, alipongeza jitihada za
watendaji wa Mradi huo unaomilikiwa na wazawa wazalendo kwa asilimia mia
moja, kwa ubia kati ya Isinka Federation 2014 Mining Cooperative
Society Limited na Kampuni ya kitanzania ya Busolwa Mining Limited.
Alisema kuwa, jitihada zinazooneshwa na
wajasiriamali hao wazalendo zinapaswa kuigwa na watanzania wengine kote
nchini kwani Mradi huo una maendeleo ya kuridhisha na kujivunia
japokuwa bado haujaanza uzalishaji.
“Sisi kama Serikali tunafarijika
sana tunaposhuhudia wananchi wazalendo wakiweka jitihada na kufanikiwa
katika biashara za madini kama hivi mnavyofanya ninyi. Tunaahidi
kuendelea kuwasaidia kadri iwezekanavyo ili muweze kufikia malengo yenu
na kuchangia katika kuinua uchumi wa nchi.” alisema Mchwampaka.
Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (mwenye koti), akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Mradi wa Uchimbaji wa Kati wa Madini ya Dhahabu uliopo Ishokelahela wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza na Maafisa wa Wizara ya Nishati na Madini, mara baada ya kukagua Mgodi huo.
Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa
Mradi huo, Baraka Ezekiel na Mrisho Masebu, waliahidi kuendelea kufanya
kazi kwa bidii na kwa ubunifu ili mafanikio yao yaweze kuwahamasisha
watanzania wengine.
Aidha, waliahidi kuendelea kutoa
ushirikiano kwa Serikali kadri ipasavyo ikiwa ni pamoja na kulipa kodi
zote stahiki pamoja na kufuata kanuni na sheria za madini zilizowekwa
kwa mujibu wa sheria.
Kamishna Mchwampaka pia alipata fursa
ya kuwatembelea na kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela
pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Samwel Sweda ambapo
walikubaliana kushirikiana katika majukumu mbalimbali yanayohusu sekta
ya madini kwa manufaa ya wananchi.
Hii ni ziara ya kwanza rasmi ya kikazi
kwa Kamishna wa Madini, Mhandisi Mchwampaka tangu alipoteuliwa na Rais
John Pombe Magufuli, kushika wadhifa huo, takribani miezi minne
iliyopita.
Kamishna Mchwampaka anaendelea na ziara yake, ambapo katika siku ya pili atazuru Mkoa wa Geita.
No comments:
Post a Comment