KAZI imeanza sasa! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya kiungo mpya wa Yanga raia wa Congo, Papy Kabamba Tshishimbi, kujiunga na timu hiyo jana Jumanne, tayari kwa kuanza majukumu yake ya kuitumikia katika michuano ya Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Tshishimbi ambaye Yanga imemsajili hivi karibuni akitokea Mbabane Swallows FC ya nchini Swaziland, ametua jijini Dar es Salaam, juzi jioni na jana asubuhi akajiunga na kikosi cha timu hiyo huko kisiwani Pemba kilipopiga kambi yake ya kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba itakayofanyika Agosti 23, mwaka huu.
Hata hivyo, Tshishimbi amewataka wapenzi na mashabiki wa Yanga
kutulia na kutokuwa na hofu yoyote dhidi yake kwani amekuja kufanya
kazi na hamhofii mchezaji yeyote atakayekutana naye uwanjani.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika, alisema kuwa kutokana na maneno hayo ya Tshishimbi, wachezaji wa Simba wakiwemo Mganda, Emmanuel Okwi na Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, wajiandae kukumbana na kazi pevu katika mechi ya Ngao ya Jamii itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
“Tshishimbi tayari ameshatua nchini na leo hii
asubuhi (jana) atajiunga na timu huko kisiwani Pemba kwa ajili ya
maandalizi yetu ya ligi kuu lakini pia mechi yetu ya Agosti 23, mwaka huu ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba.
“Mara baada ya kutua nchini Tshishimbi ametuambia
kuwa amekuja kufanya kazi na siyo jambo jingine na hamuhofii mchezaji
yeyote yule kwani anajiamini kuwa yupo vizuri kutokana na uzoefu mkubwa
katika mchezo wa soka alionao.
“Kwa hiyo wapinzani wetu wajiandae kukumbana naye uwanjani na Mungu
akipenda kazi yake ataanza kuifanya dhidi ya Simba kwa hiyo akina Okwi na Nyonzima wajiandae tu kukabiliana naye,” alisema Nyika
No comments:
Post a Comment