Na Saleh Ally
HAKUNA
anayeweza kukataa kwamba Watanzania wamekuwa wakililia sana kuona
Tanzania inakuwa na wachezaji wengi wanaocheza nje ya nchi yetu.
Wadau
wanaamini hilo ni sehemu ya kujifunza mambo mengi na kuwasaidia
wachezaji kujua mambo mengine mapya ambayo wakirejea nayo nyumbani, basi
yataanzisha mbio mpya ya mabadiliko ya soka hapa nchini.
Ingekuwa
inawezekana wachezaji wengi wa Tanzania wakaenda kukipiga Ulaya hiyo
ingekuwa bora zaidi, lakini si vibaya hata kama wataanzia nchi za jirani
kabla ya kupiga hatua zaidi kwenda huko.
Tumeona
kwa Mbwana Samatta ambaye amepata mafanikio na TP Mazembe ya DR Congo,
sasa anapiga hatua kwenda mbele. Ninaamini Watanzania wana matarajio
makubwa na Thomas Ulimwengu pia.
Wako
Watanzania wengine ambao pia tunaamini wana nafasi ya kwenda nje ambako
tunaamini kunaweza kutusaidia kwa wachezaji wetu kujifunza mambo mengi
ikiwemo nidhamu, upendo wa kimichezo, malengo na mengine mengi.
Nimeamua
kuandika makala haya baada ya kushangazwa na rafu mbili tu za mkongwe
Henry Joseph ambaye mimi nimemuona akicheza akiwa kinda hadi sasa
anajulikana kama mkongwe.
HENRY J WAKATI AKIWA SIMBA, HAPA ILIKUWA MECHI DHIDI YA MTIBWA |
Nakumbuka
alikuwa akicheza Simba wakati huo anatokea Shule ya Sekondari ya
Makongo. Alikuwa akionekana ni mchezaji ambaye atafanya vema baadaye.
Kocha wake Mbrazili wakati huo alisisitiza hilo, tena akisema Tanzania
itaweza kufanikiwa kama itawajali na kuwapenda wachezaji makinda.
Kocha
huyo aliwahi kusisitiza, kwamba amekuwa akizungumza na wachezaji
wakongwe kuwajali wachezaji makinda ili waweze nao kupiga hatua. Labda
kabla ya kueleza ninachotaka kusema, nimkumbushe hilo Henry, kwamba
lazima awajali wachezaji makinda kama ambavyo yeye wakongwe walivyomjali
wakati ule.
Ingawa
ni rafiki yangu, lakini niende mbele zaidi na kumueleza kwamba katika
mechi ya kwanza, ilikuwa Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga, Kombe la
Mapinduzi, nilishuhudia Henry akitolewa nje kwa kadi nyekundu, dakika
chache baada ya kuwa ameingia uwanjani.
HANRY J WAKATI AKIKIPIGA NORWAY |
Alilambwa
kadi nyekundu, baada ya kadi ya pili ya njano, safari hii akiwa
amemparamia kiungo Salum Telela wa Yanga. Hakika ilikuwa ni faulo ya
uchezaji wa mchangani au uswahilini kwetu ambayo isingeonekana ya ajabu,
lakini ingelalamikiwa.
Faulo
hiyo ilionyesha kabisa, Henry aliruka kwa makusudi kwenda kumkanyaka
Telela na wala hakuwa na nia ya kumzuia au kuchukua mpira.
Ilinishangaza, lakini nikaona huenda ni ubinadamu, kila mmoja anakosea.
Lakini
ndani ya wiki moja, Henry amerudia jambo kama lile lililonishangaza.
Safari hii katika mechi dhidi ya Simba Uwanja wa Taifa, juzi. Henry
alilambwa kadi nyekundu kwa kumrukia teke la Kung Fu kiungo kinda wa
Simba, Ibrahim Ajib, kabla ya hapo alimkanyaga kwa makusudi na kumuumiza
Peter Mwalyanzi.
Ajib
alitolewa nje akiangua kilio, sijui ni kwa nini. Huenda alikuwa shabiki
wa Henry wakati akicheza Simba na yeye bado akiwa shule anasoma. Sasa
anahuzunishwa na namna alivyogeuka ‘mnyama’ kwake na kumrukia mgongoni
kama mtu aliyetamani kusimamisha ndoto zake za kuendelea kucheza soka!
Usisahau,
kabla ya hapo, Henry alimrukia tena beki kinda wa Simba, Mohammed
Hussein ‘Tshabalala’ ambaye alilala chini akigugumia maumivu. Bado
ilionekana haikuwa rafu ya bahati mbaya au mtu aliyekosea kitu, badala
yake lilikuwa ni pigo la shabaha.
Mapigo
matatu ya Henry ndani ya wiki moja tena yote kwa wachezaji makinda
yananishangaza. Ninashindwa kujua kusudio na wala siwezi kukubali jambo
la bahati mbaya badala yake nabaki najiuliza, “hivi Henry hapendi
vijana, au Henry ana chuki na vijana!”
Henry
alianzia kinda kwenda kuwa mkongwe, sasa wamemkosea nini vijana, sehemu
ambayo hata yeye alipita? Lakini nikawa najiuliza, nini faida ya
kucheza soka Ulaya? Maana Henry alicheza nchini Norway kati ya wachezaji
wa Tanzania wanaotokea Ulaya kuja kuichezea timu ya taifa.
Ana
mambo mawili makubwa tayari ambayo yangemfanya uchezaji wake uyatoe
kama ushahidi. Kwanza ni ukongwe, lazima angekuwa mfano na mfano mzuri
kwake ni Shabani Nditi ambaye ni nahodha wake, ninaamini unanielewa
vizuri.
Pili, kacheza Ulaya; sasa ilimsaidia nini kama anachoonyesha hajali kuumiza wenzake, hajali kuwakatisha vijana ambao ndiyo wanaanza kupigania kutimiza ndoto zao. Hajali kutolewa nje kwa kadi nyekundu na kuisababisha Mtibwa kucheza pungufu. Ukongwe wake na kucheza kwake Ulaya, faida yake nini sasa!
No comments:
Post a Comment